Mwalimu : Apostle Daniel Stanslaus
Bwana Yesu asifiwe,
1samweli 17: 4 ( Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja.)Maandiko yanamuelezea kuwa Goliath alikuwa ni shujaa mwenye uzoefu wa vita,jasiri asiyeogopa na anayejua kutumia silaha vizuri.Goliath alikuwa na uwezo wa kupigana na mtu yoyote na asipigwe bali akashinda na ndio maana alikuwa na ujasiri wa kutukana majeshi ya Israeli .
(1samweli 17: 10 Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.).Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana. Ushujaa wa Goliath uliwafanya waisrael pamoja na Mfalme wao Sauli kuogopa na kushindwa kujitokeza mbele kupigana na Goliath, kwa hiyo maneno ya Goliath yaliwatisha waisrael wote
Goliath wa leo ni lile jambo ambalo linaitoa furaha yako, ni lile jambo ambalo ukilifikiria tu amani inatoweka ndani yako, inawezekana unatafuta kazi kwa muda mrefu,inawezekana kuna kitu unasubiri Mungu afanye,inawezekana pia Goliath akawa ni yale maneno ya kukukatisha tamaa ambayo unakutana nayo katika mazingira ambayo upo,Goliath ana sura ya kutisha katika maisha yako na anapokuwa yupo mlangoni lazima apoteze hata ibada yako na Mungu.Mtu anaweza akawa yupo kanisani lakini akifikilia jambo fulani labda hana pesa basi hata anakosa amani na wala hamsikilizi tena mchungaji.lakini pia mtu anaweza akawa yupo kanisani anasali vizuri akapokea na upako ila akirudi nyumbani na kukutana na Goliath basi amani yake inatoweka.Goliath anaweza pia kutokea hata katika ndoa,unakuta mwanandoa mmoja ametekwa na ibilisi sasa anafanyika kama Goliath kwa mme wake au mke wake.Goliath aliwafanya waisrael washindwe kuchukua hatua ya kwenda kupigana na wafilisti, na ndivyo ilivyo leo Goliath wako anapochukua nafasi kubwa katika akili yako na moyo wako sio rahisi kusikia Mungu anasema nini juu ya hiyo vita na matokeo yake kila siku utakuwa ukifikiria jinsi ya kupambana nae badala ya kusonga mbele,usipokuwa makini na Goliath anaweza akapoteza ibada yako na Mungu.
Sio kama Mungu alishindwa kumpiga Goliath kwa kutukana majeshi ya Israel,Mungu angeweza kufanya hivyo lakini alijua kuwa uwezo wa kumpiga Goliath ulikuwemo ndani ya kila mwisrael lakini kwa kuwa walitanguliza woga wakashindwa kujiamini na kusimama kupigana na Goliath,Mungu anaporuhusu Goliath katika maisha yako anajua kuwa uwezo wa kupambana na Goliath(tatizo lako) upo ndani yako, hivyo basi chukua hatua,simama,jiamini huku ukimtanguliza Mungu na utashinda.
JINSI YA KUMSHINDA GOLIATH
utaweza kumshinda kwa msaada wa Mungu aliye hai kwa hiyo mtegemee Mungu na kwa kufanya hivyo utamruhusu Mungu atawale kwenye vita iliyo mbele yako, ukimtumaini Mungu yeye anaingilia kati na atapigana kwa ajili yako 1samwel 17:38,39(Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii.Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua.)
Unatakiwa umjue Mungu unaemtumikia,ukijua ukuu wa Mungu utakuwa na Imani isiyoyumbishwa,elewa kuwa Mungu ni mkuu Zaidi ya hayo unayopitia 1samwe17:37( Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.)
Unatakiwa ujue kuwa shetani hawezi kukushinda bali anakutisha ili aitikise Imani yako na hatimaye hofu iingie ndani yako ndipo apate nafasi ya kukushinda 1samw 17:24 ( Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.)
Unatakiwa ujue kuwa Nguvu ya ushindi ipo ndani yako kwa sababu asili yako ni Mungu 2Tim1:7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni