Bwana Yesu asifiwe,
Katika somo tulilojifunza lenye kichwa kinachosema “Kwa nini sadaka nyingi za watu zinaenda kwenye dini, na siyo kwa Mungu,” nilikupitisha kwenye maandiko na kukuonyesha kuwa kuna utofauti kati ya utoaji sadaka Kibiblia na kidini. Hivyo siyo kila sadaka inaenda kwa Mungu.
Kitu cha muhimu ni kutambua ya kuwa Kanisa halikupewa torati ya Musa. Amri ambayo sisi tumepewa ni kumpenda Mungu kwa roho yote, kwa moyo wote, na kwa akili zote; na jirani kama nafsi zetu (Mathayo 22:36—40).
Hivyo msingi wa sadaka tunazotoa unatakiwa kuwa ni moyo wa upendo. Kama upendo kwa Mungu na jirani zetu haupo, Mungu hapokei sadaka.
Umewahi kujiuliza kwa nini Agano Jipya halijasisitiza sana juu ya utoaji sadaka kama Agano la Kale? Hii ni kwa sababu kusudi la Injili ya ufalme ni ili mimi na wewe tufanane na tuweze kuenenda kama Yesu alivyoenenda (Warumi 8:29; Waefeso 4:13; 1 Yohana 2:6).
Yesu alitumia muda wake kuhubiri Injili ya ufalme kuliko kuhimiza utoaji sadaka, na mitume walifanya vivyo hivyo. Hii inatuambia kuwa kwa Mungu, sadaka siyo kipaumbele cha kwanza bali mahusiano yetu na Yeye kwanza. Hivyo ukiona sadaka inahimizwa kuliko watu kumpokea Yesu, hiyo siyo Injili.
Yesu aliwaambia Mafarisayo “Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka” (Mathayo 9:13). Hii haina maana hatutakiwi kutoa sadaka, lakini upendo wetu kwa Mungu ni wa muhimu zaidi. Tukimpenda Mungu na kuishi katika pendo lake, tutamtolea kutoka katika mioyo iliyo safi na Mungu atapokea sadaka zetu.
Kanisa lilivyozidi kukua na Injili ikawafikia watu wa mataifa, neno linatuambia baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walianza kuwaambia watu kushika torati ya Musa (Matendo 15:5).
Lakini ukiendelea kusoma, mitume walisema, “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu” (Matendo 15:28—29).
Nataka uone kuwa mitume hawakusema, “ni lazima ulete fungu la kumi la mapato yako kanisani.” Kwa bahati mbaya maeneo mengi watu wanapoenda kanisani, kitu cha kwanza kinachosisitizwa ni zaka.
Pia ni muhimu kufahamu “nani anayetakiwa kutoa sadaka kwa Mungu.” Kwa wale ambao wamekulia katika mazingira ya kidini/kidhehebu, hili somo linaweza kuwapa shida kidogo kwani linaweza kuwa tofauti na mapokeo yao.
Lakini kama tunataka kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na kuurithi ufalme wake, lazima tuishi sawasawa na neno lake, na siyo mapokeo ya watu au ya dini. Ukisoma Agano la Kale, Mungu hakuwa anachukua sadaka kutoka kwa mataifa. Katika Agano Jipya, hatuoni mitume wakichukua sadaka kutoka kwa watu ambao hawajampokea Yesu.
Hivyo wale ambao hawajampa Yesu Maisha yao, hawatakiwi kutoa sadaka kwani Mungu hazipokei. “Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya” (Methali 21:27). Kabla mtu hajatoa sadaka, lazima amjue na kumpenda Mungu; na kumpenda jirani pia.
Ndio maana Yesu alisema, kama jirani yako ana neno juu yako, usitoe sadaka mpaka kwanza umepatana naye ndipo unaweza kutoa (Mathayo 5:23—24). Hii ni kwa sababu kama una shida na jirani, Mungu haipokei sadaka yako.
Kupokea sadaka kutoka kwa mataifa haipo kwenye Biblia. Huu ni mfumo ambao baadhi ya dini zinatumia “kukusanya pesa.” Siyo kila pesa inayotolewa ni sadaka kwa Mungu. Ukisoma utoaji wa Kornelio, ambaye alikuwa bado hajaokolewa na Yesu neno linasema:
Kornelio alikuwa “mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima” (Matendo 10:2). Unaweza kuona moyo wa huyu mtu ulikuwaje mbele za Mungu.
Ndio maana inapofika kwenye utoaji sadaka katika Agano Jipya, Mungu anaangalia moyo wa mtu. Tunaona mfano huu kwa mjane ambaye alitoa senti mbili lakini Bwana Yesu alisema alitoa kuliko wote (Luka 21:1—3). Hivyo wanavyohesabu sadaka duniani na mbinguni ni tofauti.
Inapofika kwenye sadaka, Mungu anaangalia moyo wa mtoaji. Paulo aliandika, “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2 Wakorintho 9:6—7).
Kuna utofauti kati ya “sadaka” na “msaada.” Kama moyo wako hauko kwa Mungu, usitoe sadaka kwani Mungu haipokei. “Msijidanganye, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna” (Wagalatia 6:7). Ndio maana Kaini alitoa sadaka na Mungu akaikataa (Mwanzo 4:3—7). Pia soma Matendo 5:1—10.
Leo tuangalie mfano wa sadaka ambao huwa ina maswali mengi kuliko sadaka zingine kwani asilimia kubwa huwa inafundishwa kidini, na siyo kibiblia. Binafsi kabla sijampa Yesu maisha yangu, sikuwahi kutoa zaka. Baada ya kuokoka, ndipo nilianza kutoa zaka. Hata hivyo nilikuwa natoa “kidini” kutokana na nilichosikia watumishi wanafundisha.
Lakini jinsi nilivyozidi kuutafuta uso wa Bwana na kutaka kuelewa zaidi, ndipo Mungu alinipitisha kwenye maandiko taratibu nikaona kumbe “sikuwa natoa zaka” bali “nilikuwa napeleka asilimia kumi ya mshahara kanisani.” Wengi huwa wanafanya hivi wakidhani wanatoa zaka kwani hata mimi nimetoka huko.
Haya ni maandiko ambayo huwa tunayasikia sana yakitumika inapofika kwenye sadaka ya zaka:
“Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam [taifa] hili lote” (Malaki 3:8—9).
Ni vizuri kuelewa kuwa hapa Mungu alikuwa anasema na taifa la Israeli. Pia ni muhimu kufahamu kuwa kanisa siyo taifa la Israeli. Ukiendelea kusoma neno linasema:
“Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika [nyumba yangu], mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la” (Malaki 3:10).
Hii [nyumba yangu] ambayo Mungu anasema SIYO Kanisa au huduma za watumishi. Hata mimi zamani nilidhani hivyo. Kumbuka Kanisa limeanza baada ya kufufuka kwa Yesu. Kwa hiyo, katika Malaki 3:10, Mungu hakuwa anasema na Kanisa.
Kama Mungu alikuwa anasema na kanisa, nina swali kwa wale ambao wamekuwa wakitoa zaka kwa uaminifu kwa kutumia maandiko haya. Je madirisha ya mbinguni yalifunguliwa na Mungu akakumwagia baraka HATA ISIWEPO NAFASI YA KUTOSHA? Kama jibu ni hapana, kwa nini?
Ningependa nije kupata ushuhuda hata wa mtu mmoja ambaye amekuwa akitoa zaka na baada ya hapo, madirisha ya mbinguni yalifunguliwa mpaka akakosa nafasi ya kuweka sawasawa na Malaki 3:10 inavyosema.
Watumishi wengine wanasema, madirisha hayakufunguliwa kama neno linavyosema kwani watu hawakutoa [zaka kamili]. Maana yake hata wao hawakutoa zaka kamili.
Hii haina maana usitoe zaka, ila usitoe zaka kwa mtazamo wa Malaki 3:10 kwani Mungu hakuwa anasema na kanisa bali wana wa Israeli. Kwa watu wengine, hili somo linaweza kuwa jipya na gumu na maombi yangu kwako Roho Mtakatifu akusaidie uweze kuelewa maandiko.
Mahali pengine wamekuwa wakihubiri/kufundisha kuwa “zaka unapeleka mahali unaposali” na hivyo kuna watu wanadhani majengo wanayokutana jumamosi/jumapili ndiyo [nyumba ya Mungu] inayoongelewa katika Malaki 3:10, ila siyo kweli.
Sasa unaweza kuelewa kwa nini umekuwa ukitoa zaka kwa moyo mmoja kabisa lakini madirisha ya mbinguni hayakufunguliwa na ukamwagiwa baraka hata ukose nafasi. Badala yake, mara kwa mara tunasikia maneno kama haya: “zaka natoa vizuri lakini mambo yangu hayaendi kabisa.”
AINA TATU ZA ZAKA NA MAKUSUDI YAKE.
- ZAKA YA MLAWI: “Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania. Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote” (Hesabu 18:21, 24).
Zaka hii ilitolewa kwa mara ya kwanza pale Abrahamu alipompatia kuhani wa Mungu Melkizedeki fungu la kumi (Mwanzo 14:18—20). Hii ilikuwa inasimama badala ya zaka ambayo wana wa Israeli watawapa Walawi kwa ukuhani wao.
- ZAKA YA KULA MBELE ZA BWANA: “Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shambani mwaka baada ya mwaka. Nawe [utakula mbele za BWANA], Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai zako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng’ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima” (Kumbukumbu 14:22—23).
“Na njia ikiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia BWANA, Mungu wako; ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; na zile fedha zitumie kwa chochote itakachotamani roho yako, ng’ombe, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako chochote; nawe utakula huko mbele za BWANA, Mungu wako; tena furahi, wewe na nyumba yako; na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe” (Kumbukumbu 14:24—27).
Nataka uone maagizo ya Mungu juu ya hii zaka na nani ambaye anaitumia. Hii ni zaka ambayo inatolewa hivyo. Kama mahali ambapo Mungu ameagiza ni mbali, neno linasema, basi mtu aibadilishe kuwa fedha na azitumie zile pesa kununua chakula ambacho mtu anapenda mwenyewe.
Hii siyo zaka ambayo anapewa mtumishi wala Kanisa lolote na inatumika kwa ajili ya kuila sikukuu. Na KUSUDI la hii zaka ni “ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima.”
Haya ni maelekezo ambayo Mungu alikuwa anawapa wana wa Israeli, na siyo kanisa. Hivyo hutasikia hii zaka ikifundishwa kwani mtoaji anaweza kuwa na uhuru wa kuamua aitumie kununua nini na kwenda kuila mahali Mungu atakapoweka jina lake.
- ZAKA YA “MIAKA MITATU:” “Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo” (Kumbukumbu 14:28—29).
Kumbuka Mungu alikuwa anawaambia wana wa Israeli alisema waiweke ndani ya malango yao kwa ajili ya kuwasaidia wajane, yatima, wageni, na maskini.
Na hii ndiyo zaka pekee, ukilinganisha na hizo za juu, ambayo kusudi lake ni “ili kwamba BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.” Sasa unaweza kuelewa kwa nini unapokuwa unasaidia maskini, wajane, na yatima kwa moyo wote, Mungu anabariki kazi yako.
SWALI: Mpaka hapa, naamini swali ulilonalo ni hili: JE ZAKA NINAYOTAKIWA NIPELEKE NINAPOSALI NI IPI?
Biblia haijasema juu ya kupeleka zaka kanisani. Ndio maana kila zaka inapofundishwa makanisani, watatumia maandiko ambayo Mungu alikuwa anawaambia wana wa Israeli. Mitume hawakufundisha juu ya zaka kabisa.
Yesu pia hakufundisha juu ya zaka. Kuna sehemu moja tu alipowaambia Mafarisayo, na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache” (Mathayo 23:23). Pia soma Luka 11:42.
Kitu ambacho Yesu alikuwa anawaambia Mafarisayo hapa ni kwamba baada ya mambo makuu ya sheria, wanatakiwa watoe zaka. Kumbuka Yesu alikuwa anawaambia watu ambao wako chini ya sheria ya Musa, na siyo kanisa. Mimi na wewe hatupo chini ya sheria. Kwa wale ambao wanatoa zaka chini ya sheria wanalaaniwa kama wasiposhika sheria zingine.
“Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye” (Wagalatia 3:10).
Kwa hiyo, kama ukiishika sheria ya utoaji zaka na ukawa unatoa kama sheria, maana yake lazima ushike zile sheria zote zaidi ya 610 zilizoandikwa kwenye torati. Neno linasema, “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote” (Yakobo 2:10).
Ndio maana mimi na wewe tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu hatuko chini ya sheria, bali chini ya neema (Warumi 6:14). Hivyo unapotoa zaka, usitoe kama sheria kwa mtazamo wa Agano la Kale. Ukifanya hivyo unajiweka chini ya laana usipoweza kushika sheria zote.
Turudi kwenye Malaki 3:8—10. Kama unaamini haya maneno Mungu alikuwa anasema na kanisa, basi tafuta sababu kwa nini pamoja na utoaji wa zaka kwa mtazamo huo hujamwagiwa baraka mpaka ukose nafasi.
Badala yake tunachoona kwa watu waliokoka na wanaotoa zaka kwa uaminifu hizi baraka za Malaki 3:10 hazipo kama wengi wanavyofundishwa. Pia [Nyumba ya Mungu] iliyotajwa katika maandiko haya siyo kanisa. Mungu hakai kwenye majengo yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu (Matendo 7:48).
Hii haina maana huwezi kupeleka zaka kanisani. Mungu akigusa moyo wako hata kupeleka 50%, tii sauti ya Mungu na peleka kwa moyo wote.
Agano la Kale linachofanya ni kutusaidia kuelewa jinsi Mungu alivyokuwa akishughulika na watu wake. Agano Jipya, ni tofauti kabisa na Agano la Kale (Yeremia 31:31—32). Shida ni kwamba watu wanajaribu kuishi chini ya torati. Wanachofanya ni kumuongeza Yesu pia.
Tunapomtolea Mungu sadaka yoyote, tunatakiwa tuitoe kutoka kwenye moyo wa upendo kwani upendo ndio ulifanya Mungu amtoe Yesu (Yohana 3:16). Kuna watu wanatoa zaka kama kifungo kwani wanaambiwa “usipotoa unamuibia Mungu na hivyo unakuwa umelaaniwa.”
Hata mimi nilikuwa naamini hivyo lakini ni muhimu kuelewa katika Malaki 3:10, Mungu hakuwa anasema na kanisa. Kama angekuwa anasema na kanisa, tungeona zile baraka za Malaki 3:10 zikitimia.
Hivyo kibiblia, Malaki 3:10 haituambii fungu la kumi la mapato yako yote peleka mahali unapoenda kusali mara moja kwa juma. Haya maandiko yamekuwa yakitumiwa tofauti ili watu wapeleke asilimia kumi ya mapato yao kanisani. Kupeleka fungu la kumi kanisani siyo vibaya lakini sicho Malaki 3:10 inatuambia.
Kwa wale wanaosema, lazima kutoa zaka kanisani kama ilivyoandikwa kwenye torati, kwa nini sheria zingine hawazishiki? Unaweza kusema, Yesu alipokufa, sheria iligongomewa msalabani (Wagalatia 3:13).
Sasa kwa nini sheria ya utoaji zaka yenyewe haikugongomewa msalabani? Kwenye dini nyingi, zile sheria ambazo zinakufanya upeleke pesa makanisani hazikugongomewa msalabani na inabidi zishikwe, lakini siyo kweli.
Sheria ambazo hazikugongomewa msalabani ni zile za kwenye amri 10. Yesu alipoulizwa na mtu mmoja “nifanye nini ili nipate uzima wa milele?” alimjibu ndani ya zile amri kumi. “Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na Mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 19:18—19).
Ndio maana Torati yote na Manabii inaangukia katika amri mbili tu: kumpenda Mungu kwa roho yote, kwa moyo wote, kwa akili zote, kwa nguvu zote; na jirani kama nafsi yako (Mathayo 22:37—40).
Hivyo msingi wa utoaji sadaka katika Agano Jipya ni MOYO WA UPENDO. Nje ya hapa Mungu hapokei sadaka. Kama upendo haupo kwa Mungu, zaka na sadaka zingine zote hazina maana mbele za Mungu na mwisho wa siku mtu ataenda jehanum ya moto.
Tuzidi kuwaombea watumishi wa Mungu ili waifundishe kweli ya Mungu jinsi ilivyo kwani neno linasema, “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi” (Yakobo 3:1).
Ubarikiwe,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni