Breaking

Jumamosi, 6 Juni 2020

Somo : Kutembea Na Mungu


Bwana Yesu asifiwe.
Ninakukaribisha tena kwa siku nyingine ambapo leo tutajifunza njia zitakazokusaidia uweze kutembea na Mungu katika maisha yako.

Kutembea na Mungu ni ile hali ya kuwa pamoja na Mungu ,ukishirikiana nae na uwepo wake kuwa na wewe siku zote za maisha yako.Pia kutembea na Mungu ni kuwa pamoja na Mungu katika kila hatua unayopitia katika maisha yako,kama vile huzuni,furaha,kwenye mapito,kwenye mateso,kwenye majaribu na katika hali zote.Ili maombi yako yapate kibali mbele za Mungu na yaweze kujibiwa kwa wepesi ni lazima ujifunze na ujue namna ya kutembea na Mungu.


Kama ukiwa unamkumbuka Mungu tu wakati wa mateso na wakati wa raha unamuacha bado hujajua kutembea na Mungu,kwa sababu ukimuacha naye anakaa mbali na wewe.( warumi 1:28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu kwenye fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizo faa, wayafanye yasiyowapasa.)

Zipo kanuni ambazo ukizifuata zitakusaidia kutembea na Mungu katika maisha yako,ambapo mojawapo ya  kanuni hizo ni  kumjua Mungu.Katika maisha ya mwanadamu ili mtu fulani awe rafiki yako wa karibu ni lazima umjue vizuri, ujue rafiki yako anapenda vitu gani na anachukia vitu gani.usipojua rafiki yako anavopenda sio rahisi kuwa rafiki yako wa karibu. .(Ayubu 22:21 mjue sana Mungu,ili uwe na amani:Ndivyo mema yatakavyokujia) Kumjua Mungu ni ile ya kujua Mungu anataka ufanye nini katika maisha yako ya kila siku.Ayubu alimjua vizuri Mungu ndio maana hata wakati anapitia magumu hakumkufuru Mungu bali alisonga mbele huku akijua ya kuwa mapenzi ya Mungu hayawezi kuzuiliwa na chochote.
Kanuni nyingine itakayokusaidia wewe utembee na Mungu ni kuwa unatakiwa umuulize Mungu kabla hujafanya chochote katika maisha yako.Mungu anapenda umtegemee yeye kwa chochote unachofanya na unachotaka kufanya, hapendi utumie akili yako,anapenda umuulize kabla haujafanya maamuzi yoyote katika maisha yako.Unapomuuliza Mungu maana yake ni kuwa unatambua kuwa pasipo Mungu wewe huwezi chochote. unapomuuliza Mungu atakupa akili na maarifa yatakayokusaidia katika safari yako au katika mambo unayotaka kufanya.

(2samweli 5: 17  Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. 18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. 19 Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. 20 Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. 21Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali.
22Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. 23Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. 24Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. 25Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama BWANA alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.)Ukisoma hayo maandiko utaona kuwa japokuwa Daudi alipakwa mafuta na Mungu kama mfalme wa Israeli lakini bado alimuuliza Mungu kabla hajaingia vitani kupambana na adui zake, ambapo kwa kufanya hivyo kila vita alishinda.Nguvu ulizonazo,upako ulionao na pesa ulizonazo haziwezi kukusababishia ushinde katika vita unayopitia au changamoto unayopitia katika maisha yako,lakini utaweza kushinda pale tu utakapomuuliza Mungu kabla ya kuchukua maamuzi yoyote.


Kanuni Nyingine itakayokufanya uweze kutembea na Mungu ni kukubali na kutii maagizo ya Mungu kupitia watumishi wake na kupitia Neno lake. Isaya 1:19 (kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi).Wakati Mungu anamkabidhi Yoshua aliongoze kundi la waisrael alimpa maagizo ambayo utayaona katika kitabu cha Yoshua(Yoshua 1: 8  Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana)Kwa kutii maagizo hayo Yoshua aliwafikisha waisrael kunapo kusudi, kwa hiyo unapofuata maelekezo ya Mungu unaruhusu uwepo wa Mungu kutembea na wewe  kwa kuwa Mungu ni Mungu wa agano.
MUNGU AKUBARIKI SANA

Apostle  Eng.Daniel  Stanslaus
Contact: Whatsapp +255756277095

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni