Bwana Yesu asifiwe.
Ninakukaribisha tena siku nyingine tuweze kujifunza Neno la Mungu.Na siku ya leo tutajifunza somo linalosema KUVUKA BAHARI YA SHAMU
Katika Biblia,bahari ya Shamu ni ile bahari ambayo ilikuwa kizuizi kwa wana wa Israel kuelekea katika ile nchi ya Ahadi. Baada ya Taifa la Israel kukaa utumwani kwa muda mrefu Farao aliwaruhusu waondoke lakini cha kushangaza ilifika mahali wana wa Israel baada ya kuruhusiwa wakawaona tena askari wa Farao wakiwafuatilia kwa nyuma na sio hivyo tu mbele ya wana wa Israel kulikuwa na bahari ya Shamu.Walibaki wakihuzunika sana katika mioyo yao kwa sababu
Kutoka 14:9-12 ( Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana.Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.)Waisrael walipoona kuwa hakuna njia ya kukimbilia hofu iliwaingia na wakaanza kumlalamikia Musa, walifikiri kuwa Mungu aliyewatoa utumwani amewaacha waangamie jangwani,walisahau kama Mungu yupo pamoja nao na ndio maana walikuwa wakiongozwa na wingu mchana na usiku kama nguzo ya moto.Hofu iliwafanya wasahau wema na fadhili za Mungu katika safari yao.
Kazi kubwa ya shetani ni kukuwekea mazingira magumu katika njia yako ili ukikutana na hayo mazingira usahau kumuangalia Mungu,uanze kulia,kukata tama,kunung’unika, na hatimaye urudi nyuma na usiendelee mbele .Shetani anajua wazi kuwa ukisongambele utafika katika utukufu na baraka ambazo Mungu amekuandalia katika maisha yako.
Hivyo unapokutana na hali ngumu katika maisha yako tofauti na matarajio yako unatakiwa uelewe kuwa njia za Mungu hazichunguziki na Mungu anaweza kufanya njia hata pale pasipokuwa na njia.Isaya 55:9 (Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.)Mungu aliwaahidi wana wa Israel kuwa atawapeleka katika ile nchi ya ahadi, kwa hiyo Mungu alijua kuwa kuna mazingira magumu watakutana nayo na Mungu mwenyewe alikuwa anajua namna ya kuwapitisha katika hayo mazingira kwa kuwa tayari alikusudia kuwafikisha katika nchi ile ya ahadi.
Unatakiwa usimame,uwe imara usiogope hali yoyote ngumu unayokutana nayo kwa kuwa Mungu atawaangamiza adui zako wote wanaotaka kukuangamiza na hatimaye utafika katika mafanikio yako ambayo ndiyo nchi yako ya ahadi
Mungu akubariki sana.
Apostle Daniel
Whatsapp +255756277095
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni