Breaking

Jumatano, 24 Juni 2020

Somo : Heri Wenye Moyo Safi


Bwana Yesu asifiwe
       Ninakukaribisha tena siku ya leo tuweze kujifunza Neno la Mungu.Leo tutajifunza somo zuri lenye kichwa cha habari kinachosema Heri wenye moyo safi.
        Moyo ni kiungo muhimu sana katika mwili wa Mwanadamu.(Mithali 4:23 .Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.) Maandiko yanaonyesha kuwa uzima wa mwanadamu asili yake ni moyo na ndio maana Neno la Mungu linasema tulinde sana moyo kuliko yote tuyalindayo.Ili Uwe na mafinikio ya kiroho na kimwili ni wajibu wako kuulinda sana moyo wako kuliko chochote.Usiishi maisha ya kutosamehe ,usitunze maumivu  na vidonda
moyoni mwako,ishi maisha ya furaha hata kama unapitia magumu kwa sababu ukifanya haya moyo wako utakuwa na furaha sana na kamwe moyo wako hautolala.( Mithali 17:22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa) maandiko yanaonyesha kuwa moyo wenye amani na furaha huwa unachangamka na kusababisha tiba ya mambo mbali mbali katika maisha yako.
Ukiwa na amani moyoni mwako sio rahisi kuwa mtu wa kuumwa mara kwa mara kwa kuwa amani ya moyo ni tiba kamili.Lakini kama moyo wako una maumivu ni rahisi sana kupata magonjwa mengi na hatimaye yanaweza sababisha kifo.(Mithali 13:12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.) maandiko haya yanaonyesha kuwa watu wengi wameingia katika maumivu pale wanapochelewa kupata majibu yao tofauti na walivotarajia, na ndio maana maumivu hayo ya moyo yamewafanya kuchukua maamuzi mabaya ambayo mwisho wake ni anguko na mauti.Usiruhusu maumivu moyoni mwako pale unapotengwa,unapoachwa, unapokuwa huna pesa, na pale unapopitia changamoto mbalimbali.Moyo wako ni wa muhimu na ni wa thamani sana kuliko changamoto unayopitia,ipo gharama kubwa kuurudisha moyo katika hali yake ya kawaida pale unapokuwa na majeraha.Kwa hiyo ndugu yangu nakushauri kuutunza sana moyo wako.
       Sababu kubwa ambayo inawafanya watu kuumia mioyo ni kukosa shukrani mbele za Mungu.(Zaburi 103:1-2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote).Moyo wako unapojawa na shukrani hata upitie changamoto kubwa  sio rahisi kuogopa na kuumia bali utamshukuru Mungu na kusonga mbele.Unatakiwa ujue kuwa Mungu anakulinda na mengi sana ambayo  wewe huyajui na ndio maana hadi leo bado uko hai kwa hiyo Mungu ana mpango mzuri na maisha yako

      Mathayo5:8(Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.) maandiko yanaonyesha kuwa ili uweze kumuona Mungu katika maisha yako kwa lolote lile unalofanya unatakiwa uwe na moyo safi kwa kuulinda moyo ili hali yoyote ya kuumiza isikae ndani ya moyo wako.(Mithali 12:25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha) uzito katika moyo wako unatokana na kuhifadhi vitu vingi katika moyo wako kama vile dhambi,maumivu kutokusamehe na vingine vingi ambavyo matokeo yake husababisha moyo kulala na moyo unapolala uwepo wa Mungu unatoweka katika maisha yako na hatimaye mlango wa kuingiza mapepo unafunguka katika maisha ya mwanadamu.Moyo wako uliumbwa kama sehemu ya kukutana wewe na Mungu wako,kwa hiyo moyo wako ni mahali pa Ibada kati yako na Mungu.Moyoni mwako usiweke chochote zaidi ya Neno la Mungu kwa kuwa ukiweka vitu vingine na vikaja kupotea moyo wako utajeruhika(Zaburi 119:11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi)
      Kama moyoni mwako kuna maumivu ninakushauri nenda mbele za Mungu umuombe ili akuponye na Mungu ni mwaminifu sana atakuponya maumivu yote yaliyo ndani ya moyo wako na atakujaza Nguvu zake ili usonge mbele.
Mungu akubariki sana
Apostle Daniel
whatsapp:+255756277095

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni