Breaking

Jumatano, 19 Agosti 2020

SOMO: JINSI YA KUTEMBEA NA UWEPO WA MUNGU


MWALIMU: APOSTLE DANIEL STANSLAUS
Bwana Yesu asifiwe
        Ninakukaribisha tena tuweze kujifunza Neno la Mungu.Siku ya leo tutajifunza somo linalosema JINSI YA KUTEMBEA NA UWEPO WA MUNGU.Uwepo  wa Mungu ni mazingira yaliyojaa Nguvu ya Mungu.Kwenye uwepo wa Mungu kuna Mungu mwenyewe  pamoja na Nguvu zake.Uwepo huu wa Mungu upo kwa ajili ya kutupa wepesi katika maisha yetu kwa kila jambo ambalo tunalifanya.Ikiwa unapitia mazingira magumu na kila unalofanya halifanyiki unahitaji kutembea na uwepo wa Mungu ili ukuvushe na kukupeleka hatua nyingine.(Yohana 15:5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote) maandiko yanaonyesha kuwa pasipo Bwana Yesu sisi hatuwezi Neno lolote.Katika uwepo wa Mungu kuna ustawi,mafanikio,kubarikiwa na kuinuliwa..
Zaburi 27:5 5  Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba)Maandiko haya yanaonyesha kuwa unapokuwa katika uwepo wa Mungu unapata ulinzi wa kukulinda na mabaya yote,lakini pia uwepo huo unakuinua na kukuweka nafasi za juu katika maisha yako.Ukiwa katika uwepo wa Mungu adui zako wanakuwa adui wa Mungu na hivyo Mungu anaingilia kati  vita yako na kukupatia ushindi.
        Mungu alipotuumba aliuweka uwepo wake ndani mwetu. (Mwanzo 1:26  Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.)Kinachoutoa uwepo wa Mungu katika maisha yetu ni dhambi.Mungu anataka tumpende yeye na kufuata Sheria yake ili uwepo wake uzidi kukaa ndani yetu.Uwepo wa Mungu unaweza ukautunza ndani yako na ukate,mbea nao mda wote.
        Yapo mambo ambayo ukiyafanya yatasababisha uwepo wa Mungu ukae ndani yako,ukatembea nao na usiondoke.Mojawapo ya kitu kitakachokusaidia ni kuliamini Jina la Yesu.
Marko 5:28 (maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona).Maandiko haya yanaoyesha imani aliyokuwa nayo yule mwanamke aliyetoka damu muda wa miaka 12,ambapo Imani yake ilimsababishia akutane na nguvu ya Mungu iliyomponya pale alipogusa vazi la Bwana Yesu.Imani juu ya Jina la Yesu itakupa ujasiri pale utakapokuwa ukitumia Jina hilo na kwa kuwa Mungu hupendezwa na wale wenye Imani iliyo imara basi uwepo wake utakufuata.
        Kitu kingine kitakachosababisha utembee na uwepo wa Mungu ni pale utakapokuwa na upendo .Kwa kuwa asili ya upendo ni Mungu mwenyewe basi ukiwa na upendo Mungu anaweka makazi ndani yako na uwepo wake utakuwa ukitembea nao.lakini kama hauna upendo kwa wengine Mungu anatoka katika maisha yako na giza litatawala maishani mwako.1yohana 2:11 (Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho)

Mazingira magumu unayopitia yasichukue nafasi moyoni mwako bali mtazame Yeye.ukizipa changamoto  nafasi au mazingira magumu ukayapa nafasi katika moyo wako uwepo wa Mungu unatoka(Zaburi 119:11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.).Mungu ametuumbia mioyo kwa ajili ya kutunza Neno lake tu na sio kuweka mizigo mingine kama kutokusamehe,uchungu na dhambi.ukiweka mizigo moyoni mwako sio rahisi kusikia maelekezo ya Mungu anayokupa katika kipindi kigumu unachopitia.Kumbuka kuwa katika hali yoyote mbaya au changamoto yoyote unayopitia ipo sauti ya Mungu ya kukupa maelekezo namna ya kutoka..
Unatakiwa pia ujifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie katika maisha yako.(1yohana 5:14 Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia)usiporuhusu mapenzi ya Mungu kutimia katika maisha yako utalazimisha mapenzi yako yatimie na mwisho wake utaingia kwenye uharibifu.

Ninakushauri utafute sana kutembea na uwepo wa Mungu ili uwe na Nguvu ya kukuwezesha kufanya jambo lolote katika maisha yako.Usije ukamtafuta Mungu kwa sababu tu unahitaji muujiza au usije kumtafuta Mungu kwa sababu una mahitaji yako unatamani Mungu afanye bali mtafute Mungu na kumkaribia siku zote za maisha yako.usije kuwa kama baadhi ya wanafunzi wa Yesu ambao walimtafuta Bwana Yesu kwa sababu ya ile mikate waliyopewa.(Yohana 6:26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.)
Mungu akubariki sana.
Kwa ushauri na maombezi unaweza kunipata kupitia
Mtume Daniel
Whatsapp +255756277095

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni