MWALIMU: MTUME DANIEL STANSLAUS
Bwana Yesu asifiwe.
Ninakukaribisha tena tuweze kujifunza Neno la Mungu .Leo tutajifunza somo linalosema KUISHI MAISHA YENYE MAFANIKIO.
Maisha yenye mafanikio ni yale maisha ya kumiliki,kutawala na kuongezeka hatua moja kwenda hatua nyingine ya kimaendeleo kila siku.Kusudi la Mungu kukuumba wewe ni ili umtumikie lakini pia uishi maisha yenye mafanikio na yaliyojaa amani na furaha.(Mwanzo 1:28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi)kinachosababisha wanadamu kuishi katika maisha ya mateso ni dhambi au maovu yaliyofanywa na familia zetu.Ukisoma biblia kitabu cha Mwanzo 3:24 utaona kuwa dhambi ilisababisha Adam kufukuzwa bustanini ambapo
walikuwa wakiishi maisha mazuri.( Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima) Katika maandiko haya yanaonyesha kuwa dhambi inaweza kumtoa mtu nje ya Baraka za Mungu na kumuacha mtu akiishi maisha yasiyo na mafanikio.
Ili uishi maisha yenye mafanikio unatakiwa uwe ndani ya Bwana Yesu.(Yohana 15:4-5 Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote) hauwezi kupata mafanikio kama bado hujamruhusu Bwana Yesu aingie ndani yako na kutawala maisha yako.Bwana yesu amesema katika hayo maandiko kuwa pasipo Yeye sisi hatuwezi kufanya Neno lolote.Yesu ni njia, kweli na uzima kwa hiyo akiwa ndani yako utaijua kweli lakini pia atakuonyesha njia za kufanya ili uweze kufanikiwa katika maisha yako na lolote lile utakalofanya litakuwa na uzima kwa hiyo hautofanya mambo kwa hasara.Watu wengi wamekuwa wakimkumbuka Mungu kwa kipindi cha matatizo lakini baadae wakifanikiwa wanamsahau Mungu.Unatakiwa umkumbuke Mungu na utafute uso wake siku zote za maisha yako iwe wakati wa shida au wakati wa raha.Unatakiwa ujue kuwa mafanikio yanatokana na Nguvu ya Mungu (Kumb 8:18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.). maandiko yanaonyesha kuwa Mungu ndiye anayetupa Nguvu ya kupata utajiri na kuishi maisha yenye mafanikio, kwa hiyo usije ukamwacha Mungu bali utafute uso wa Mungu siku zote ili akupe Nguvu zitakazo kuwezesha ufanikiwe katika maisha yako
Bwana Yesu anakaa ndani yako pale unaposhika amri zake (1 Yohana 3:24Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.) Kuzishika sheria za Mungu ni kufanya yote ambayo Mungu ameagiza katika Neno lake.Tena maandiko yakasema Yesu anakaa ndani yako kama Roho mtakatifu.Kwa hiyo akikaa ndani yako anaachilia Nguvu itakayokufanya ufanikiwe,lakini pia huyo Roho mtakatifu atakuongoza na kukutia Nguvu katika vipindi vyote vya maisha unayopitia iwe wakati wa raha,mateso,huzuni na kudharauliwa.Lakini pia unapofuata na kushika sheria za Mungu kumpenda Mungu kunakuwa ndani yako.kwa sababu huwezi kumpenda Mungu kama hushiki sheria zake ( Yohana 14:15 Mkinipenda, mtazishika amri zangu) lakini pia kumpenda Mungu ni pamoja na kuacha yale mambo ya dunia(1 Yohana 2:15-16. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.)Tusipopenda Mambo ya dunia Mungu anakuwa ndani yetu na kutufanya tufanikiwe.Bwana Yesu anapokuwa ndani yako anaachilia Pendo lake ambalo pendo hilo linakupa amani lakini pia linaondoa hofu na mashaka na hatimaye maisha yako yanakuwa ya kustawi.
Ndugu yangu Mungu amekusudia kukupa maisha mazuri yenye mafanikio,hakikisha unafata haya niliokuambia ili uishi maisha hayo.
Mungu akubariki
Kwa maombi na ushauri unaweza kunipata kupitia namba +255756277095
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni