Bwana Yesu asifiwe
Ninakukaribisha tena siku nyingine tuweze kujifunza Neno la Mungu.Na leo tutajifunza Somo lenye kichwa cha habari kinachosema MUNGU AMEYAJIBU MAOMBI YAKO.
Ndugu yangu,najua yapo maombi yako ambayo ulimuomba Mungu kwa muda mrefu ili afanye katika maisha yako.Inawezekana mambo yako yameenda tofauti na ulivyotarajia kadiri siku zinavyozidi kwenda.Unaweza ukawa umekata tamaa kwa kusubiri mda mrefu bila kupata majibu.Leo nakuhakikishia kuwa Mungu tayari ameyajibu maombi yako.
Yohana 14:13-14 ( Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.)katika maandiko haya Mungu amesema tena mara mbili kuwa tukiomba lolote kwa Jina la Yesu atalifanya.Chochote kile ulichoomba Mungu amesikia na amefanya tayari katika ulimwengu wa roho na muda si mrefu utaona matokeo katika ulimwengu wa mwili.Tabia ya shetani ni kukupa mawazo mabaya ili akukatishe tamaa na kuuharibu mtazamo wako juu ya Mungu na kukufanya uone kuwa ahadi za Mungu sio za kweli.Shetani anayafanya haya kwa kuwa hapendi mwanadamu amtegemee Mungu na kumsubiri.Kumbuka kuwa siku zote shetani ni Muongo na kawaida yake ni kupinga kweli ya Mungu.(Waefeso 4:27 wala msimpe Ibilisi nafasi)Maandiko yanaonyesha wazi kuwa tusimpe ibilisi nafasi katika maisha yetu,usimpe nafasi ya kukuletea mawazo mabaya ya kukukatisha tamaa.Siku zote elewa kuwa Mungu ni mwaminifu sana hawezi kusema uongo, kama amesema atajibu maombi yako basi elewa kuwa hakuna kitakachomzuia yeye kukujibu maombi yako, hakikisha kwamba umeomba maombi ambayo yatampa Mungu utukufu.
Hesabu 23:19 ( Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?)Maandiko yanasema kuwa Mungu sio mwanadamu na anachosema kinafanyika kwa hiyo siku zote za maisha yako mchukulie kuwa Mungu ni mwaminifu na kwa kufanya hivyo utayaona majibu yako yale uliyomuomba Mungu.(Waebrania 11:11 Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu) katika maandiko hayo yanaonyesha kuwa Mungu tayari alisema kuwa atampa Sara mtoto na kilichomfanya Sara apokee majibu yake ni kitendo chake cha kumchukulia Mungu ni mwaminifu.Ili uyaone majibu yako baada ya kumuomba Mungu unatakiwa umchukulie Mungu kama ni mwaminifu, pasipo kuangalia changamoto unazopitia.
Usiache kumngoja Bwana endelea kumsubiri kwa kuwa ameshajibu maombi yako na muda wako ule uliopendezwa naye wa kuyaona hayo majibu uliyoomba unakuja nawe utamfurahia Mungu na kumtukuza na kumrudishia utukufu wote.
Mungu akubariki sana
Kwa ushauri na maombi unaweza kuwasiliana na mimi kupitia
Mtume Daniel,
Email:danielstanslaus@gmail.com
Whatsapp: 0756277095
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni