Bwana Yesu asifiwe
Ninakukaribisha tena siku ya leo tuweze kujifunza somo lenye kichwa cha habari kinachosema,NGUVU ITENDAYO KAZI NDANI YAKO
( Mwanzo 1:26 )Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi)Sisi wanadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,asili yetu ni Mungu.Mungu alipotuumba alituwekea Nguvu ndani yetu ambayo Nguvu hiyo ndiyo inayoweza kutufanya tumiliki na kutawala hapa Duniani.(Kumbukumbu la torati 8:18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo)Maandiko haya ya kumbukumbu la torati yanaonyesha kuwa hata utajiri unatokana na Nguvu ambayo ipo ndani ya mtu na anayetoa hiyo Nguvu ni Mungu
mwenyewe.Mtu asipomiliki na kutawala ni matokeo ya kuikosa ile Nguvu ya Mungu.Ni wewe ndiye unayeweza kusababisha Nguvu hiyo ifanye kazi ndani yako au isiwepo kabisa ndani yako.(Mithali 10:4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha).maandiko haya katika kitabu cha mithali yanaonyesha kuwa uvivu unaleta umasikini na uvivu ni matokeo ya kukosa Nguvu ya Mungu ya kukupa utajiri.Nguvu ya Mungu ya kukupa utajiri inapokuja ndani yako huwa inaondoa uvivu.
Waefeso 3:20 Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;)Mungu anaweza kabisa kufanya mambo makubwa na ya kushangaza katika maisha yetu,lakini anafanya hayo kwa kadiri ya Nguvu iliyo ndani yako.Kwa hiyo sasa kiwango cha Nguvu ya Mungu iliyo ndani yako ndicho kwa kiwango hicho hicho Mungu atafanya na kuonekana katika maisha yako.Na ndio maana watu ambao kila kitu wanasema hawawezi maisha yao huwa ni ya kiwango cha chini na wale watu wanaopenda kuthubutu huwa wana maisha mazuri.
Yapo mambo ambayo ukiyafanya yatasababisha Nguvu ya Mungu iliyo ndani yako ifanye kazi kwa kiwango kikubwa na kuruhusu Mungu afanye mambo makubwa na ya kushangaza katika maisha yako.Jambo mojawapo ni Imani.Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.Unapokuwa na hakika kuwa Mungu atafanya yale mambo uliyoyaomba,Imani hiyo itasababisha Nguvu iliyo ndani yako ifanye kazi kwa kiwango kikubwa,na ni kwa sababu Mungu hupendezwa na wale watu wenye imani.(Waebrania 10:38 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye).Ukiwa na Imani utamfurahisha Mungu naye ataruhusu Nguvu yake ndani yako itakayokufanya ushinde,umiliki na kutawala.
Jambo lingine ni Kusubiri.Unapokuwa na moyo wa kusubiri kwa lile jambo ambalo umemuomba Mungu, Mungu huruhusu Nguvu yake ndani yako ikufanye uzidi kusonga mbele lakini pia hiyo Nguvu inakufanya upate majibu yako na inakufanya ufanye vitu vikubwa na vya kushangaza.(Isaya 40:31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia) maandiko haya ya Isaya yanaonyesha kuwa wale wanaomsubiri Mungu ndio wanaopewa Nguvu ya kufanya mambo makubwa.Subira ni kitu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu,subira humfanya mtu asichoke hata kama amesubiri kitu kwa mda mrefu sana, na watu wanaosubiri ndio hao Mungu huwa anawajibu na kuwapa kumiliki,ambapo mfano mmojawapo ni Ibrahimu.Aliweza kupata mtoto kwa kuwa alisubiri, kwa hiyo kwenye kusubiri pana majibu yako.
Jambo lingine ni kiu iliyo ndani ya moyo wako.Kiu iliyo ndani yako ya kutamani jambo fulani Mungu alifanye kwako humfanya Mungu aachilie Nguvu ya kukufanya ufanikiwe kulipata hilo jambo.(Ufunuo 21:6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure) Kwa hiyo unapokuwa unatamani jambo fulani Mungu alifanye kwako,hali hiyo ya kutamani itakufanya umsogelee Mungu kwa kuutafuta uso wake ambapo kwa kufanya hivyo Mungu anakuwa anafurahishwa na wewe na hatimaye anaruhusu ushinde na upate majibu yako.
Unatakiwa pia Neno la Mungu lijae kwa wingi ndani yako ili Nguvu ya Mungu ndani yako ikupe kushinda na kukufanya umiliki na kutawala.Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe lakini pia Neno la Mungu ni taa ya njia zetu, lakini pia ni Nuru.Neno la Mungu likijaa kwa wingi ndani mwako Nuru ya Mungu itajaa ndani yako ambapo itakufanya uweze kupita hata katika mahali pa giza na pale pasipokuwa na njia na mwisho wake utauona utukufu wa Mungu ukijifunua katika maisha yako.
(Yoshua 1:8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana)kitabu hiki cha Yoshua kinaonyesha kuwa Neno la Mungu likijaa kwa wingi ndani yako na ukaenenda sawa sawa na Neno,Mungu atakupa nguvu ya kukufanikisha katika njia yako au katika mambo unayofanya.
Ndugu yangu kuanzia leo tambua kuwa Nguvu ya Mungu ipo ndani yako ambapo ipo tayari kukufanikisha na kukupa maisha mazuri yenye mafanikio.Amua leo kufanya hayo niliokueleza ili Umuone Mungu katika maisha yako
Mungu akubariki sana
Kwa maombi na ushauri wasiliana name kupitia
Mtume Daniel
Whatsapp: +255756277095
Email:danielstanslaus@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni