Mwalimu : (Apostle Eng Daniel Stanslaus )
Bwana Yesu asifiwe.
Leo ni siku nyingine ambayo tunakwenda kujifunza kuwa Mungu anakwenda kuifuta Aibu uliyoipata katika maisha yako.
Aibu ni matokeo ya Uthamani wako, heshima yako au utu wako kupotea mbele za watu ambapo inasababishwa na kushushwa kutoka katika hali ya juu na kupelekwa katika hali ya kiwango cha chini; lakini pia aibu ni matokeo ya utukufu wa Mungu kupotea katika maisha yako.
Biblia inaeleza kuwa chanzo cha aibu ni pale mwanadamu anaposhindwa kufuata sheria za Mungu.Unapoenda kinyume na Maagizo ya Mungu fahamu kabisa kuwa uwepo wa Mungu katika maisha yako unaondoka na kukuacha peke yako na unapoachwa peke yako lazima aibu itakukuta katika maisha yako. Biblia inaeleza kuwa asili ya aibu ilikuwa ni pale kwenye bustani ya Eden ambapo iliwapata Adam na Eva..
Mwanzo 3:7 (Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo).Adam na Eva walipata aibu pale bustanini baada ya kutofuata maagizo ya Mungu kwa kula matunda ya mti wa katikati ambao Mungu alikuwa amewakataza.Kwa kutokufuata maagizo ambayo Mungu aliwapa walijitoa wenyewe katika ile nafasi ambayo Mungu alikuwa amewaweka na ndio maana Mungu alipokuwa anatembea bustanini alianza kuwaita kwa kuwa hawakuwepo katika nafasi waliyopewa..Mwanzo 3:9 ( Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?) Dhambi inakutoa katika nafasi ambayo Mungu amekuweka na matokeo yake ni kushushwa kutoka katika nafasi ya juu na kuwekwa nafasi ya chini na ndipo aibu inakufata.Aibu haiwezi kukupata kama utakuwa karibu na Mungu na kufuata maagizo yake.
Usipofuata maagizo ya Mungu ,Mungu anakukataa na ukikataliwa na Mungu sio rahisi mwanadamu akukubali.
Kukataliwa na Mungu kunaambatana na kushushwa kutoka katika nafasi uliyokuwa nayo. 1samweli 15:26 (Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.) Mfalme Sauli alikataliwa na Mungu kwa sababu hakufuata maagizo ya Mungu aliyopewa na matokeo yake ni kutolewa katika nafasi ya Ufalme na Daudi akawa mfalme wa Israel.
Je umepata aibu katika maisha yako? Ofisini kwako, kwenye ndoa yako, kwenye biashara yako na kwenye familia yako? Je shetani amefanikiwa kukutoa kutoka katika kibali na Neema ambayo Mungu aliachilia kwako?
Nina habari njema kwako siku ya Leo kwamba Mungu anakwenda kufuta aibu uliyoipata katika maisha yako, Mungu anakwenda kukufuta machozi, Mungu anakwenda kukuheshimisha na kurejeza uthamani wako uliopotea kutokana na aibu uliyoipata.
Unachotakiwa kufanya ni wewe kurudi mbele za Mungu na kuomba Toba na msamaha pale ulipofanyika chanzo cha kujisababishia aibu yako kutokea.
Tambua kuwa baada ya toba Mungu atakusamehe na kusahau dhambi zako lakini pia mahusiano yako na Mungu yanarudi tena na hapo ndipo Mungu anakuinua tena kutoka kwenye aibu na kukuweka mahala pa juu na heshima yako kurejeshwa tena. Mithali 28:13 (Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.)
Kwa hiyo bado hujachelewa nenda mbele za Mungu omba toba na rehema hakika Mungu anakwenda kukuinua tena na kurudisha heshima yako iliyopotea.
Mungu akubariki sana.
CONTACT: WHATSAPP +255756277095
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni