Breaking

Jumamosi, 12 Januari 2019

Salamu na Maombi ya Mwaka Mpya Kwako

Salamu na Maombi
Tumuinue Mungu wa mbinguni na Bwana wetu Yesu Kristo kwa kutuwezesha kuingia mwaka mpya wa 2019.
Katika mwaka 2019, Maombi yetu kwako ni Mungu akusaidie katika vipengele 19 vifuatavyo:

1. Tafuta ufalme wa Mungu kwanza kuliko vitu vingine vyote.
Katika mwaka huu, fanya ufalme wa Mungu uwe kipaumbele cha kwanza na Mungu atakupatia mahitaji yako.
“Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33).
2. Tafuta kusudi la Mungu kwako kwa mwaka 2019, lifanye hilo kwa viwango vya Mungu, na limalize.
“Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yohana 4:34).
3. Mpende sana Mungu na neno lake likae ndani yako.
“Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23).
“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote” (Wakolosai 3:16a).
Yesu alisema, “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana 15:7).
Tukimpenda Mungu kwa roho zetu zote, kwa mioyo yetu yote, kwa akili zetu zote, na kwa nguvu zetu zote, hapo ndipo tunaweza kumpenda jirani kama nafsi zetu.
4. Tafuta kujua tabia ya Bwana Yesu na kuenenda kama Yeye alivyoenenda.
“Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda” (1 Yohana 2:6).
5. Tafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu na kumpenda Mungu na siyo kutafuta kuwapendeza wanadamu.
Wanaongia katika ufalme wa mbinguni ni wale ambao wanayatenda mapenzi ya Mungu (Mathayo 7:21b).
“Kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu” (Luka 16:15b).
6. Tafuta kuishi maisha ya utakatifu na siyo maisha ya dhambi. Hii ndiyo njia kubwa ya kumshinda Shetani.
“Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi” (1 Yohana 5:18).
7. Zifahamu njia ambazo Mungu anasema nawe kupitia maono, ndoto na njia zingine. Fahamu alama za siri za Biblia ambazo Mungu anazitumia kusema nawe.
Kuisikia sauti ya Mungu ni muhimu sana hasa katika hizi nyakati za mwisho. Pia kuna kunena kwa lugha ambako kunafumbua mafumbo ya Mungu pasipo adui kuyajua.
“Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake” (1 Wakorintho 14:2).
Pia Mungu anaposema kupitia ndoto na maono, kuna alama anazitumia ili kwamba wewe unayepewa ujumbe uweze kuelewa. Hivyo muombe Mungu uweze kuelewa (Mwanzo 40:8).
8. Omba pasipo kuchoka; soma na tafakari sana neno la Mungu.
Yesu “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaaa” (Luka 18:1).
“Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku” (Zaburi 1:2).
9. Ongeza kutenda wema kwa watu, hasa kwa maskini, yatima, na wajane.
“Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua” (Waebrania 13:2).
Abraham alikaribisha wageni na kuwahudumia kumbe walikuwa malaika na wakamletea habari njema kwake (Mwanzo 18).
Mungu anataka tuwajali na kuwasaidia wenye mahitaji (Kumbukumbu 15:11; Zaburi 68:5).
“Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu” (Waebrania 13:16).
10. Tafuta kuweka hazina mbinguni, siyo duniani, na tafuta mambo yaliyo juu Kristo alipo.
“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi” (Mathayo 6:19—20).
“Basi mkiwa mefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi” (Wakolosai 3:1—2).
11. Safisha hekalu la Mungu ili Roho Mtakatifu akae (Marko 11:15—17; 1 Wakorintho 6:19).
12. Mruhusu Roho Mtakatifu akuongoze katika njia zako zote.Yeye atakusaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika maisha yako ambayo yanamrudishia Mungu utukufu.
“Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Warumi 8:14).
13. Kuwa tayari kwa ujio wa Bwana Yesu wakati wote.
“Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja” (Mathayo 24:44).
“Bali ninyi, ndugu, hamno gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi” (1 Wathesalonike 5:4).
14. Heshimu na tii mamlaka ya serikali. Kutokutii mamlaka ni kutokumtii Mungu.
“Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu” (Warumi 13:1—2).
Nakuombea kwamba katika mwaka 2019, nuru yako iangaze kwa watu (Mathayo 5:16).
15. Jitenge na watumishi wa uongo: manabii wa uongo, mitume wa uongo, waalimu wa uongo, wachungaji wa uongo, na wainjilisti wa uongo ambao wanadanganya watu kwa jina la Yesu.
“Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi” (Mathayo 24:5).
Jitenge na watumishi wa uongo ambao mkazo wao upo kwenye ishara na miujiza na siyo kwenye neno la Mungu.
“Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata walio wateule” (Mathayo 24:24).
16. Linda sana moyo wako kutoka katika udanganyifu binafsi (self-deception)
“Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua” (Yeremia 17:9).
“Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchem za uzima” (Methali 4:23).
17. Komboa wakati. Tumia muda wako kuyatenda mapenzi ya Mungu na siyo katika mambo yasiyofaa.
Moja ya njia ambayo adui anatumia ili kuwazuia watu wasiweze kutimiza mapenzi ya Mungu ni kuuteka muda wao.
“Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo, msiwe wajinga, bali myajue ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana” (Waefeso 5:15—17).
18. Fanya Maombi (Omba) na muulize Mungu akuongoze ni watu gani wa kushikamana nao.
Kuna marafiki ambao wapo kwa ajili ya kukwamisha kufikia kusudi ambalo Mungu amelikusudia katika maisha yako.
“Ajifanyiaye Rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko Rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu” (Methali 18:24).
19. Fanya Maombi (Omba) nafsi itakaswe na kufanywa upya kwa neno la Mungu na usifikiri kama ulimwengu unavyofikiri.
Kwa kufanya hivyo, utaweza kuyajua yaliyo mapenzi ya Mungu katika maisha yako.
“Wala msiifuatishe namna ya duni hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hatika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu” (Warumi 12:2).
Yesu alisema, “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kwel” (John 17:17).
Tunawatakia heri ya mwaka mpya na wenye baraka 2019. Maombi yetu kwako ni kwamba tunapozidi kuikaribia dhiki kuu, utaweza kuvumilia mpaka mwisho na kutopoteza imani kwa Bwana Yesu.
“Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mathayo 24:13)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni