Breaking

Alhamisi, 3 Januari 2019

Fahamu Mambo Au Mazingira Yanayoweza Kufanya Ukatenda Dhambi



UTANGULIZI.
Lazima tujue mazingira au ushawishi unaoweza kumsababisha mtu atende dhambi au amkosee Mungu. Si kila mahali au kija jambo linaweza kukutoa katika uwepo wa Mungu, ila yapo mambo au mazingira ambayo humpelekea mtu kutenda dhambi, iwe kwa kudhamiria au kwa nguvu ya 
ushawishi. Na pia si kila mtu anayetenda dhambi kwamba anafurahia, hata makahaba na walevi wa kupindukia tunaowaona si wote wametaka au wanafurahia hali zao, ila kuna mazingira yanayowapelekea kuwa hivyo walivyo. Katika Warumi 7:15 inasema
Maana sijui nifanyalo, kwasababu lile nilipendalo, silitendi, bali nilichukialo ndilo ninalolitenda.
Unaweza ukatamani sana sana kumpendeza Mungu na kukaa uweponi mwake wakati wote, lakini kila ukijitahidi unashindwa, unashangaa mara limetokea hili na lile umemtenda Mungu dhambi. Na yale ambayo hupendi wala huyawazii kuyatenda ndiyo unaanza kuyatenda kila siku, Je, ni kwa nini sasa? Ni mambo gani yanasababisha uwe mtu wa kuanguka dhambini kila mara?
1. Kutokuwa na Msingi wa Neno la Mungu.
Kutokujihusisha na neno la Mungu humaanisha ya kwamba kuna mwongozo mwingine unaotegemea katika maisha yako ambao kwa hakika lazima utaangukia DHAMBINI TU.
Daudi anaandika katika
Zaburi 119:105
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Tunapojikita katika kusoma Neno la Mungu tunapata kufunuliwa mambo kadha wa kadha na kukaa uweponi mwa Mungu, na kinyume chake ni kuyumbishwa katika upepo wa kila namna. Katika Hosea 4:6 Neno linasema
Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe…
Neno la Mungu linakutosheleza katika kutimiza mahitaji yako ya kila siku na wakati huo huo kutulia uweponi mwake katika hali ya Utakatifu, Lakini kwa kukosa/kukinai neno tunaangukia dhambini.
2. Hasira.
Hasira imepelekea watu kujiua, kufukuza wake zao au waume zao, kutukana, kufanya vurugu na maovu mengineyo. Na kwakutambua hilo Biblia haikuacha kusema hilo ndio maana katika Waeféso 4:26 inasema
Mwe na hasira, ila MSITENDE DHAMBI, jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.”
Ni kweli huwezi ukazuia hasira, na haikwepeki, kuna mambo yanakera kabisa, ikiwemo ya mambo ya kusingiziwa, n.k lakini bado tunapewa onyo HASIRA HIZO ZISITUPELEKEE kumtenda Mungu dhambi. Epuka kufanya jambo au maamuzi yoyote ukiwa na hasira, hyo itakusaidia usitende dhambi.
3. Kuongozwa na mwili.
Maandiko yanasema siku zote nia ya mwili ni mauti, usitegemee hata siku moja mwili wako utakusukuma kumpendeza Mungu. Hujawai ona kuna kitu unasukumwa sana kukifanya ndani lakini mwili wako hautaki kabisa? Je, hatujawahi kusoma kuwa Roho i radhi lakini mwili ni dhaifu? unaweza ona vile mwili unapingana na mapenzi ya Mungu. Katika Wagalatia 5:16 Neno linasema
Basi nasema, ENENDENI KWA ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
Mwili siku zote umejawa na tamaa, pia hapo hapo neno linasema tamaa ni dhambi, tunaweza ona vile ilivyo muhimu kuenenda katika Roho na kuongoza na Roho katika mambo yote.
NA SI ROHO TU, BALI ROHO MTAKATIFU, KWANI KUNA ROHO YA SHETANI PIA.
4. Ushawishi wa wenye dhambi.
Usitegemee mtu aliyezoelea dhambi akakushawishi wewe mazuri ya kumpendeza Mungu, yawezekana wewe kimbilio lako la kwanza ni kutaka ushauri au kuambatana na watenda dhambi, sasa lazima ipo siku watakuangusha dhambini tu. Katika Mithali 1:10 Inasema
Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali.
Mungu anajua kabisa wenye dhambi ni watu wenye kushawishi wengine kuanguka nao dhambini, na kamwe hawawezi kukuelekeza katika njia ya haki, hujawahi ona kama ni mlevi anamshawishi mtu asiyemlevi akimwambia, “onja tu kidogo”? hayo yote ni ushawishi wa wewe kuanguka dhambini. Kuna mazingira ya ushawishi unaweza ukayaepuka, na kama hayaepukiki basi JENGA MSIMAMO UNAPOSHAWISHIWA USIKUBALI.
5. Majaribu.
Majaribu ni kizuizi au kifungo fulani katika maisha ya mtu. Na watu wengi wameshindwa kuwa wavumilivu kusubiri wakati wa Bwana na kuamua kupita njia za mkato. Kuna wengine kwa kukosa kazi muda mrefu, wamekua tayari kuuza miili yao au kutoa rushwa za namna nyingine ili mambo yao yaende vizuri, wakisahau Wanamtenda Mungu dhambi kwa ajili ya mambo ya kitambo. Lakini Neno lasemaje katika Ufunuo 2:10 Inasema
Usiogope mambo yatakayokupata, tazama, huyo ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakua na dhiki siku kumi, UWE MWAMINIFU HATA KUFA, NAMI NITAKUPA TAJI YA UZIMA.
Mkazo wangu ni hapo nilipoandika kwa herufi kubwa, ya kwamba tuwe waaminifu katika kumtazama Mungu, haijalishi tunachoka na kuumia kiasi gani, tuwe waaminifu mpaka kufa, wala shida na taabu hizo zisitufanye tumtende Mungu dhambi.
KILA JARIBU UNALOPITIA LINA MLANGO WA KUTOKEA, WALA LISIKUSABABISHE UMTENDE MUNGU DHAMBI.
6. Kuendekeza mizaha.
Mizaha na utani vimesababisha wengi kupigana, kuchomana visu, na vurugu za namna mbalimbali. Wengine wameshindwa kustahimili hasira za mizaha wakaangukia katika matusi na visa. Katika Zaburi 1:1
Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia ya wakosaji, WALA HAKUKETI BARAZANI PA WENYE MIZAHA.
Biblia inamuita mtu asiyeketi barazani pa wenye mizaha kuwa HERI kwake. Maana katika mizaha kuna mengi, na shetani hutumia njia hiyo kupoteza wengi, wengine siku ya tar 1/4 wanaiita sikukuu ya wajinga, wanaitumia kudanganyana, hivi mfano Mungu akishuka siku kama hiyo umeshadanganya watu kwa mzaha mzaha hatahesabu uongo huo kama dhambi? Au uongo wa siku hiyo sio dhambi? Msisitizo wangu ni kuwa makini na mizaha, usiipe kipaombele sana, kwani ni mlango wa wazi sana ambao shetani huutumia kupotosha wengi.
7. Kulewa vitu (ulevi wa vitu).
Ulevi si lazima iwe pombe, unaweza ukapata kitu kikakulewesha akili zako zote na mategemeo yako yote yakahamia hapo. Kuna watu walimlilia Mungu kwa ajili ya kazi au kupandishwa vyeo baada ya kupata walivyoomba wakaaza kulewa kwavyo. Na matokeo ya kulewa huko ni kutenda dhambi kuona huitaji kingine chochote uko huku kufanya unachojisikia, ile hofu ya Mungu haipo tena kwani ulikua nayo kipindi cha uhitaji, baada ya kupata ukajisahau. Katika 1 Wafalme 11:4 neno linasema
Maana ikawa, Sulemani alipokua mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.
Tunaweza kusema kuwa Sulemani alijichimbia kaburi la uharibifu mwenyewe, alifika mahali akaona anajitosheleza kwa kila kitu,akajitwalia wanawake wengi kadri alivyoweza huo ndio ukawa ulevi wake. Na mwishowe alimtenda Mungu dhambi kwa kuigeukia miungu mingine.
UNYENYEKEVU ULIOKUA NAO WAKATI WA DHIKI ISIFIKE WAKATI UKAJISAHAU UONE UMEFIKA, KUANGUKA KU KARIBU KULIKO KUINUKA.
8. Kukosa Nguvu za Roho Mtakatifu.
Kamwe akili zetu, wala fahamu zetu haziwezi kutusaidia tusimtende Mungu dhambi, ila tukiwa na Nguvu za Roho Mtakatifu sawa na Matendo 1:8tutaweza. Yesu mwenyewe alitambua hatuwezi ndio maana akatuachia msaidizi. Katika Yohana 14:16-17 Inasema
Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakua ndani yenu.
Roho Mtakatifu ndiye pekee anayeweza kumsaidia mtu asitende dhambi. Ataachilia hofu ndani yako, (hofu ya kumuhofu Mungu), pia ataongoza hatua za miguu yako yaani uende wapi na usiende wapi, pia atakupa maneno ya kuzungumza au kutamka, ukiwa na nguvu za Roho Mtakatifu hauwezi kuwa mropokaji wa ovyo wala mtukanaji, kwa maana hata maneno ya kinywa chako yataratibiwa naye.
SISEMI KWA HABARI YA ROHO MTAKATIFU, BALI NASEMA KWA HABARI YA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU, MAANA KAMA NI KUJAZWA ROHO MTAKATIFU WENGI WALISHAJAZWA LAKINI BADO WANAENDELEA NA DHAMBI. (Matendo 1:8)
9. Kukosa hazina ya Neno la Mungu moyoni mwako.
Kuna watu au niseme kuna Wakristo ambao hawana Neno kabisa, yaani mtu akisoma Biblia anasoma kama gazeti, hana muda wa kulitafakari, hana muda wakupata mafunuo juu ya neno, hana muda wakulihifadhi yaani yupo tu. Ikatokea umemnyang’anya Biblia basi kwisha habari yake. Lakini mtunzi wa Zaburi 119:11 Anasemaje?
Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako, nisije NIKAKUTENDA DHAMBI.
Kumbe Neno ndani ya moyo wake ndiyo kinga au kengele ya kumwongoza katika njia zake. Unapokua na Neno la Mungu ndani ya moyo wako unapojaribiwa kutenda dhambi daima litakukumbusha yaliyo mapenzi ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Lakini kama huna Neno utakumbuka nini sasa? Kumbuka hata Yesu alipotoka mlimani baada ya maombi ya siku 40 shetani alipomjaribu hakurudi mlimani kuomba, bali alimshinda KWA NENO, kwa kumwambia Imeandikwa… Hivyo tujizoeze kusoma Neno, kulitafakari na kulihifadhi ndani ya mioyo yetu.
Kuna mambo mengine wala hauitaji kufunga wala kuomba, UKIWA NA HAZINA NZURI YA NENO TAYARI UMESHINDA.
10. Kutokua mwombaji.
Maombi ni silaha moja wapo kati ya nyingi ambazo zinaweza kukusaidia kumpinga shetani. Ukisoma katika Waefeso 5:11 Neno linasema
Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.”
Moja ya hila ya shetani kwako ni wewe umtende dhambi. Lakini unapokua mwombaji unaachilia ulinzi wa Mungu katika maisha yako, na shetani hataweza kukuangusha kirahisi, na kuomba huko uombe kwa msingi wa Neno, usiombe tu mradi umeomba. Mfno unaweza kuomba sawa na Zaburi 119:37
Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako.
Macho nayo yameponza wengi kumtenda Mungu dhambi, ata mwizi aliona kwanza ndipo akaiba. Mzinzi na mwasherati aliona, akatamani kisha akaanguka dhambini. Pia ombea miguu yako, ifungiwe utayari katika kupeleka habari njema za Ufalme, na wala isikumbilie masengenyo wala kupeleka maneno ya uchonganishi na ufitinishi.
11. Kukinai au kukosa makusanyiko ya watakatifu. (Waebrania 10:25)
Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine, bali tuonyane, na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa imekaribia.
Katika kukusanyika kama watakatifu, kuna kufundishana, kuonyana, na kutiana moyo katika changamoto mbalimbali ili tuweze kuimarika katika Kristo na kudumu katika UTAKATIFU.
MJUE SANA MUNGU ILI UWE NA AMANI, NA NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUJILIA.
Hitimisho
Nipende kusema kuwa si hayo tu bali hayo ni baadhi tu. Yapo mambo mbalimbali na mazingira yanayoweza kukuangusha dhambini, hivyo tia bidii katika kusoma NENO LA MUNGU na kufwatilia Watumishi wa Mungu mbalimbali kwa msaada zaidi. Naomba kuhitimisha katika kitabu cha Yohana 4:34
Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, NIYATENDE MAPENZI yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.
Chakula ni kitu muhimu sana katika maisha ya Mwanadamu, huwezi kuishi bila chakula. Yesu akachukulia namna hiyo kwa kusema “Chakula chake ni kuyatenda mapenzi ya baba yake.” Yaani kila siku imempasa kutenda mapenzi ya baba yake, ni bora akose vyote lakini ayatende mapenzi ya baba yake. Kwa maana mapenzi ya Mungu siku zote ni mazuri na makamilifu, hayana dhambi ndani yake, bali yamejaa UTUKUFUU NA THAWABU nyingi. Je, mimi na wewe chakula chetu ni nini? Pia Paulo mtume anatusisitiza haya katika Wafilipi 4:8
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli,yoyote yaliyo na staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema, ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo.
“NIKUSHUKURU SANA KWAKUA PAMOJA NAMI KATIKA SOMO HILI, NI OMBI LANGU KWA MUNGU ATUPE NGUVU YA KUISHI MAISHA YA USHINDI DHIDI YA DHAMBI KATIKA KUISHI KWETU HAPA DUNIANI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni