Neno la kusimamia
“Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika kristo, walakini HAMNA BABA WENGI. Maana mimi ndiye niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya injili”
(1Wakorintho 4:15)
Utangulizi;
Kupata baba wa kiroho sio jambo rahisi na ni jambo la nadra sana. Kwa sababu sio kila mtumishi wa Mungu ana sifa ya kuwa baba, sio kila mtu anayefundisha Neno la Mungu ni baba. Na si kila wahubiri na waalimu maarufu, wa ndani na nje ya nchi ambao wana sifa ya kuwa baba. Wala si kila nabii ana sifa ya kuwa baba, ndio maana Paulo alilieleza neno hili kwa wakorintho.
Baba ni zawadi adimu
Kutakuwa na watu wengi watakaokuwa na mchango mzuri katika maisha yako, wakufunzi na waalimu ni wengi, lakini hawa wote mchango wao ni tofauti na wa baba.
Mchango wa baba ni kamili. Baba hukupa kitu kamili ambacho kimekamilika, ni zaidi ya mafundisho mazuri.
Kwa kawaida Mwalimu anajali sana kutoa somo zuri. Wakati nabii anajali zaidi kutoa huduma yenye kuonyesha nguvu za Mungu kwa njia ya maono, ndoto na neno la maarifa. Lakini baba anajali zaidi hali ya maisha yako yote.
Kwa sababu kazi ya baba ina mambo mengi ya kumjenga mtu, ndiyo maana akina baba sio wengi!
Ni rahisi kupitia notisi zilizoandaliwa na mtumishi kuliko kutoa uangalizi kamili kwa mtu unayemlea. Watu wanaweza kuwa wagumu na wasio na shukrani kiasi kwamba ni baba tu ndiye anayeweza kuwastahimili kwa kipindi kirefu. Ni Mara nyingi walezi wamelalamikiwa na watoto wao wa kiroho kwamba ni wadhaifu katika huduma lakini walivumilia.
Kuna wachungaji, wainjilisti na manabii wengi lakini ni shida sana kumpata mwenye sifa ya kuwa baba, ndio maana Paulo alisema, “kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi”
SIFA KUU YA BABA
Sifa kuu ya baba sio umri wake bali ni uwezo wake wa kuzaa watoto wanaofanana naye. Kinyume na maoni ya watu kadhaa, kuna vijana wengi makanisani wenye moyo na sifa ya kuwa baba.
Kwa kawaida uthibitisho wa ubaba mara zote uko ndani ya watoto ambao wame zaliwa na baba, ubaba upendo, kujitoa na uvumilivu katika kulea watoto hao ndio sifa kuu ya baba. Na hatimaye watoto ndio ambao huthibitisha ubaba wako.
Eliya na Elisha.
Kama utasoma kwa uangalifu biblia na kulinganisha huduma ya Eliya na Elisha, kwa mfano utaona tofauti kubwa sana kati ya nabii mwenye sifa ya kuwa baba na nabii asiye na sifa ya kuwa baba. Tofauti hizi zinakuwa wazi zaidi unaposoma kwa makini huduma zao. Kwa kulinganisha huduma, Eliya na Elisha wote walikuwa ni manabii mahiri lakini Eliya alikuwa na karama ya nyongeza ya kuwa baba. Ndiyo maana alikuwa na mrithi wa huduma yake ambaye ni Elisha.
Elisha hakuwa na mrithi. Kwa sababu alimlaani Gehazi ambaye angekuwa mrithi wake, alimlaani kwa sababu alifanya makosa katika mambo ya fedha. Elisha alikosa uvumilivu na akaamua kuchukua hatua ya kuua kabisa huduma ya kijana wake
Moyo wa baba hauwezi kumlaani mtoto wake wa pekee. Roho ya baba ni kile kitu kinachosababisha mtu wa Mungu kuzaa watu kama yeye mwenyewe katika huduma.
Kwa maneno mengine karama ya baba ni udhihirisho wa upendo wa Mungu. Inahitajika upendo ili kuwalea watu wasioelewa ni kitu gani wanachofanyiwa.
Inahitajika upendo kuwalea watu ambao wakati mwingine hawatakuelewa pengine kwa miaka mingi kuwa wewe ni baba kwao.
Kwa kawaida, Mungu hutuma waalimu wengi sana ambao wanatuhudumia katika maisha yetu vizuri. Wanatufundisha masomo na mambo mengine muhimu sana ya mafundisho makuu yanayohusu maisha yetu. Lakini baba atakwenda hatua ya ndani zaidi. Pamoja na kukufundisha, atakuonyesha upendo na uvumilivu unaohitajika kukufikisha katika kusudi kamili la Mungu. Wakati fulani nilikwenda kwa mchungaji kumueleza tabia ya ndugu mmoja ambaye alikuwa anatia aibu kutokana na matendo yake ambapo nilikuwa ninalazimika kuutetea ujinga wake ili tusiuaibishe wokovu wetu. Nilipokwenda kwa mchungaji, nikidhani itakuwa habari mpya kwake nikakuta anajua mambo mengi kuliko Mimi, Mimi nilitaka atengwe kwa muda ili apate fundisho, akaniambia, sio kila wakati tunatumia rungu katika kulea, rungu linaua
Huwezi kupata mtoto ukamilifu bila kupitia katika Mchakato wa ukamilifu mtumishi anayetafuta mtu mkamilifu ili amlee, ujue huyo sio baba mzuri. Ni lazima tukumbuke kuwa neema ya Mungu inafanya kazi polepole katika maisha ya mtu, baba anayedhani mtoto wake ni mkamilifu wakati wote hawezi kukosea, hiyo ni ngumu sana hakiwezekani kwa binadamu mwenyewe mwili.
Kuwatambua na kuwapokea baba ambao Mungu anawatuma katika majira tofauti maishani mwetu ni jambo linalohitaji neema na ufunuo katika kuwatambua.
Mungu atakutumia baba tofauti katika nyakati tofauti kulingana na malengo na mipango yake anayokusudia kukutumia katika kufanya kazi yake.
Mungu anatujua kabla hata ya kuweka misingi ya ulimwengu ndio maana
Mungu hutuma watu kadhaa kukulea na kukuimarisha kulingana na uhitaji wa hali ya nyakati hizo.
Wa kwanza kabisa ni baba yako wa kimwili ambaye ni lazima umpokee vyema na umuheshimu. Usimuone kama mzee fulani mshamba mshamba hivi, ambaye haendani na uhalisia wa maisha yako ya kisasa unayoishi.
kumwona baba yako wa kimwili kama mtu aliyepitwa na wakati kutakuzuia kupokea mambo mengi na kupunguza siku zako za kuishi duniani, maana ipo ahadi ya Mungu ya kuongezewa siku zako za kuishi duniani kutokana na kuwaheshimu baba na mama yako waliokuzaa, pia unaweza kukosa hekima na baraka zao kutoka ndani ya mioyo yao.
Ni kweli kwamba huyu baba yako wa kimwili atakuwa na muda wa kukaa na wewe pia atakuwa na mipaka yake katika kukulea kulingana na mtiririko wa somo hili.
Lakini ghafla mwendo wa maisha yako utabadilika na utajikuta uko na mtu mwingine atakayetumwa na Bwana kuwa baba yako atajitokeza, yaweza kuwa ni kwa kupitia huduma yake utapokea malezi ya baba yaliyohitajika kuyapata katika wakati huo ili kwenda katika hatua nyingine ya maisha yako, baada ya kusudi la baba huyo kwisha hapo tena atatokea mtu mwingine atainuka na kuwa baba yako tena katika maisha yako, mbio za aina hii huendelea kama mashindano ya mbio za kupokezana kijiti, kutoka kwa baba mmoja kwenda kwa baba mwingine. Unaweza kuwa sio mtu wa usharika wenu lakini utakapokuwa unashauriana naye utatambua ana kitu fulani maalumu kwa ajili yako. Katika maisha yangu Mungu amekuwa mwema sana kwangu kwa kuniwezesha kuwatambua baba zangu mapema, na hiyo ilinisaidia kila wakati kuacha kinywa wazi kama kinda la ndege mwenye njaa nilihakikisha nanyonya sawasawa, lakini pia na Mimi Kuna watu nilijua kuwa Bwana amenifanya kuwa baba yao nilijitahidi kusimama katika nafasi yangu na nilimwona Mungu, Nina shuhuda nyingi sana ambazo katika nafasi hii hazitoshi kuweka.
Sio kila kitu baba wa kimwili anaweza kukupa.
Nimekuwa mchungaji wa kanisa la vijana wa kipentekoste na nikatamani sana kufundisha masomo yanayohusu mabadiliko ya vijana katika ukuaji wa rika, hata masomo mara nyingi hayafundishwi makanisani nililazimika baada ya kuona vijana wengi wanaangamia kwa sababu, wazazi ni vigumu sana kuongea na watoto wao kuhusu mambo yanayowakabili katika mabadiliko hayo, na nilipofundisha nikaona kama vile nimefungua milango ya gereza fulani maana vijana walikuwa na maswali mengi na nikagundua wengi walikuwa wamefungwa bila msaada. Kuna mambo mengi ambayo baba wa kimwili hawezi kukuambia. Labda na yeye angependa kukueleza kila kitu, lakini maadili yanamfanya ashindwe kufanya hivyo. Sio rahisi mzazi kukupatia ushauri wa kina wa namna ya kuchagua mke wa kuoa au mume wa kukuoa, wazazi wengi wa kimwili wanatoa maoni na ushauri tu kuhusu mambo mbalimbali katika ndoa.
Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya wachungaji ambao hupewa jukumu hili la kuwaongoza watoto katika ndoa, Mara nyingi wachungaji hawa huwa ndio wazazi wanaofuatia katika mbio hizi.
Mara nyingi nimetamani Mungu atume watu wengine kuwahudumia watoto wangu. Baba wana upeo mkubwa sana katika kujali maisha yako, mchango wao unakwenda mbali zaidi ya yale wayasemayo. Utagundua kwamba huduma yao ina matokeo makubwa na ya ajabu sana katika maisha yako.
Moja ya vigezo vya kumtambua baba ni kutambua jinsi anavyoonyesha upendo wa Baba wa mbinguni kwako, kujali kwake na mwongozo wake katika maisha yako.
Watu wengi hufikiri kimakosa maandiko yasemayo “mnao waalimu elfu kumi lakini mna baba mmoja.”
Andiko hili linasema kwamba hamna baba wengi. Kwa maneno mengine kinasema kwamba mna baba wachache.
Yesu alisema, “Wala msimuite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni” Mathayo 23:9.
Yesu alisema hivi kwa sababu anajua hakuna binadamu anayeweza kutosheleza kwa ukamilifu mtiririko huu tunaojifunza kuhusu mambo tunayopasa kufanyiwa na baba katika nyakati za maisha yetu yote ya kiroho.
Hakuna mwanadamu ambaye amekamilika katika jukumu hili, ni Baba wa mbinguni pekee ndiye ambaye hutoa kielelezo halisi cha baba.
Ni mara ngapi tumesikia jinsi baba wa duniani hushindana na kupigana na watoto wao?
Hata baba wa kimwili wanaweza kusababisha maumivu makali kwa watoto wao.
Watu wengi huwachukia baba zao. Na Kuna watu wengi ambao maisha yao yameharibika kwa sababu ya wazazi wao. Huu ni ushahidi wa kutosha kwamba kuwa baba Kwa njia ya binadamu wa kawaida Kuna mapungufu mengi hiyo ndio sababu Kuna hitajika ninachokiita “mbio za kupokezana vijiti kwa baba”.
Mbio hizi humhusisha Mungu kutuma mtu mmoja baada ya mwingine katika awamu tofauti za maisha yako na huduma yako. Ni muhimu kutambua hawa watu mbalimbali wanapokuja maishani mwako. Hiki ndicho Yesu alichokifafanua kwa mfano katika mathayo 21 hakika tutahukumiwa kwa jinsi tunavyowapokea baba tofauti wanaotumwa na Mungu kwetu.
Soma Mathayo 21:33-39
Mungu hutuma baba kadhaa katika maisha yetu na Mara nyingi hatuwafahamu, wakati mwingine watu hupigana na baba zao bila kujua! Tunapaswa kujifunza baba wanaotumwa na Mungu katika maisha yetu.
Tofauti ya kumpokea baba na kumpokea mkufunzi.
Kumpokea mkufunzi kunahusisha kupokea masomo anayotoa kutoka katika neno la Mungu, lakini kumpokea baba kunahusisha kumpokea mtu fulani ambaye huduma yake italeta uhai katika vipawa na karama zako.
Kwa kawaida baba yako wa kimwili ana mvuto mkubwa kwako kwa namna nyingi. Yeye kukufundisha namna ya kula, kuvaa kusema na kuishi. Hukupatia hekima, ushauri na masomo machache ya kuhusu maisha. Yeye huwa kielelezo cha maisha na huwa ni chanzo cha hamasa na mwelekeo katika maisha.
Tofauti na mwalimu wako wa shule, waalimu huwa hawatoi mwongozo kamili kama wanavyofanya wazazi wako.
Ukikutana na mtu mwenye mvuto mkubwa wa huduma katika maisha yako, hapana shaka kuwa umekutana na mmoja wa baba wanaotumwa na Mungu kwako.
usifanye kosa kumpokea baba kama mwalimu wa kawaida tu.
Watu wengine wanafanya makosa ya kuwapokea baba zao kama walimu wa kawaida. Kufanya hivyo unaweza kukosa kupokea sehemu ya mchango ambao Mungu alipanga utolewe na baba hawa kwako, kwa hiyo tunakuwa tumepunguza jukumu lao kwetu na kuwa kama walimu wa kawaida tu.
Kuna watu ambao Mungu alinitaka niwalee kama baba yao. Lakini nikajikuta ninahusiana nao kama mwalimu wa kawaida tu, kwa sababu wao hawakutambua na mimi nilikwenda nao vile walivyotaka.
Mathayo sura ya 21 inaonyesha wazi kwamba Mungu atatuhukumu kwa namna tunavyohusiana na watu hawa anaowatuma kwetu kama baba.
Unaweza ukapata kitabu au kanda yenye mafundisho ya mtumishi fulani na Mungu akakufungua kupitia mafundisho ya mtumishi huyo, na hapohapo akawa ni baba yako, na ukajikuta unatamani upate kila kitu kutoka kwake na kukuta unazalisha vitu vipya katika huduma yako
Mungu akubariki sana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni