Mwalimu : Apostle Daniel Stanslaus
Bwana Yesu asifiwe,
Mwanadamu anayo mawazo anayowaza juu ya maisha yake na Mungu anayo mawazo anayowaza juu ya maisha yako.Mawazo yako yanaweza yakawa chanzo cha wewe kusogea katika hatua nyingine maishani mwako lakini pia mawazo yako yanaweza yakawa chanzo cha wewe kutokusogea hatua nyingine katika maisha.Unahitaji kujua mawazo ambayo Mungu anawaza juu ya maisha yako ambapo kwa kujua mawazo hayo itakupa Nguvu ya kusonga mbele na kufikia mafanikio yako.
Ukisoma kwenye biblia Yeremia 29:11 ambayo inasema (‘’Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’’)Mungu anasema kuwa anatuwazia Mema na wala hatuwazii mabaya.Kuna mazingira magumu ambayo mwanadamu anaweza kupitia kama vile mazingira ya aibu,kudharauliwa,kuachwa, njaa,mateso,upweke,magonjwa na hata kusalitiwa ambapo mazingira haya yanaweza kumfanya mtu aone kuwa Mungu anamuwazia mabaya kwa kuruhusu hayo yatokee lakini kumbe Mungu anatuwazia Mema katika maisha yetu.
Wapo pia watu ambao wakiona maombi waliyopeleka mbele za Mungu yanachelewa kujibiwa wanaanza kuwaza Mungu amewasahau na anawazia mabaya.Kuna wakati Mungu anaruhusu hayo ili aone uaminifu wako kwake,Mungu anaangalia je hata wakati wa mateso utazidi kumpenda na kumtumaini? Kwa hiyo unatakiwa kipindi hicho cha mateso uelewe kuwa bado Mungu anakupenda na anakuwazia mema .lakini pia Kipindi hicho Mungu anakupitisha kukupeleka kwenye wazo lake zuri juu ya maisha yako.Mazingira Magumu unayopitia ni njia ya Mungu kukupeleka kwenye mafanikio yako na kwenye baraka alizoziandaa juu ya maisha yako.
Ibrahim alipitia hali ngumu ya kukosa mtoto kwa mda mrefu sana, hata umri wake aliokuwa nao ulikuwa ni mkubwa kiasi kwamba sio rahisi kupata mtoto lakini Mungu alikuwa tayari amemuahidi kuwa atambariki na kuwa baba wa mataifa.Ibrahim angeweza kuwaza kuwa Mungu anamuwazia mabaya kwa kuchelewa kumpa mtoto lakini Ibrahim hakuwaza hayo bali aliendelea kumuamini Mungu hadi wakati ulipowadia mke wake Sara akapata mtoto.
Mwanzo 12:1-2 (‘’ Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe Baraka”)Ingawa Ibrahim alipitia maumivu ya kusubiri mtoto kwa mda mrefu Mungu alikuwa anamuwazia Ibrahim kuwa atakuwa taifa kubwa,atakuwa mbarikiwa na kuwa baraka.Kwa mfano huo ninakuhakikishia kuwa Mungu anawaza mema juu ya maisha yako kwa hiyo wewe songa mbele na uamini haya na hakika Ipo siku yako ambayo Mungu atakupa lile tamanio la moyo wako.
Apostle Daniel Stanslaus
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni