Breaking

Jumapili, 17 Mei 2020

Mambo Tusiyopenda Lakini Yenye Mchango Mkubwa Katika Kustawi Kwetu ( Sehemu 2)


Mwalimu Deborah E. Lema (Mrs)

Sehemu ya kwanza ya somo hili tulipata neema ya kutazama mambo matano yenye mchango mkubwa kwenye ustawi wetu, na kwa neeema ya Mungu awamu hii tutamalizia sehemu zilizobakia (6-10). Kama ndo unasoma kwa mara ya kwanza, unaweza kuanza na sehemu ya kwanza kwa kubofya hapa


6. KULIPA GHARAMA.

Watu wanapenda mteremko. Watu wanapenda kuwekewa mikono mambo yaende chap chap, watu wanapenda kuwaeleza watu shida zao wahangaikiwe lakini wao wamekaa pembeni. Unamskia mtu anampangia mtumishi wa Mungu “naomba hili hitaji langu unisaidie kufunga tatu kavu” huku yeye anakula na kustarehe.

Ni kweli una shida, lakini umefanya kwa sehemu gani? Umewahi kufunga na kuomba Mara ngapi? Kwa wiki au mwezi unafunga Mara ngapi kuutafuta uso wa Mungu? Juu ya huduma yako, kazi, biashara, ndoa, masomo n.k ni gharama gani unalipa? Au umemwachia nani alipe gharama kwa niaba yako? Una uhakika gani kuwa uliyemwambia akubebee huo mzigo anaubeba kama vile ambavyo ungeubeba wewe? Una uhakika gani na uhusiano wa huyo mtu unayemwamini na Mungu? Mtu pekee anayeweza kujua uzito wa jaribu au tatizo lako ni wewe mwenyewe. Usipende kupata faraja ambazo hazitakusaidia.

Ni gharama gani umelipa au unalipa? Hiyo gharama unayolipa inalingana na uhitaji ulionao? Au unafanya tu kama ushahidi? Neno linasema katika Wagalatia 6:7 ya kuwa

“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi, kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”

Unataka ndoa bora unapanda nini kama sehemu ya gharama? Unataka uje kuoa au kuolewa na mtu bora na mwaminifu, wewe ni bora na ni mwaminifu? Kwa lolote unalolitamani litimie, kuna gharama ya kulipa. Ukiendelea kukaa hakuna kitakachobadilika.






7. KUANZA UPYA.

Kuanza upya si dhambi, haswa pale unapopata neema ya kutambua kuwa haukua katika njia sahii iwe kwa mambo ya rohoni au mwilini. Ile tu kutambua kuwa ulikosea ni neema, wako wanaoendelea mbele kwa mbele katika upotovu wao. Ikiwa unoana kabisa utakapoanza upya kuna mabdiliko yatatokea usiogope utaonekanaje, usiseme wataniona nimeshindwa, usiseme ntaonekana mjinga. Fanya jambo lenye manufaa. Usikubali kufa na kamba shingoni kwa kisingizio kuwa watakuonaje.

Unakumbuka kwa habari ya mwana mpotevu? Hivi angesema kuwa nikirudi kwetu ntaonekanaje hali yake ingekuaje? Angeogopa kukiri kosa na kuomba msamaha unadhani hali yake ingekuaje? Kwanini wewe unaogopa? Hata kama ulienda mbali sana pekeyako na hujapata mafanikio yoyote, usiogope kuanza upya na Bwana. Yamkini hayo unayopitia ni matokeo ya kufuata akili zako bila kumshirikisha Mungu, yamkini ni matokeo ya kushupaza shingo, omba rehema Mungu atakusamehe. Unapomaanisha ataanza nawe kama Alfa na atahitimisha kama Omega. Kama yule baba aliweza kumpokea mwanae upya (LUKA 15:11-24, MUNGU SI ZAIDI?






8. KUJIKUBALI.

Kwanini ujilinganishe na mtu? Kwanini utumie gharama kubwa kushindana na mtu? Kwanini ufanye mambo yaliyo nje ya uwezo wako matokeo yake uangukie hasara na madeni? Kila mmoja kuna upekee alionao ambao hakuna yeyote duniani alionao. Jifunze kwa mfano mdogo tu kupitia alama za vidole, haziwezi kufanana hata kama ninyi ni mapacha.

Unapoishi maisha yako halisi na kufanya mambo yaliyo ndani ya uwezo wako kwa uaminifu, unampa Mungu nafasi ya kushughulika na hali yako. Huna haja ya kujidharau na kujiona duni. Huitaji kuwa kama fulani ndipo ufanye jambo fulani. MUNGU ATAJIPATIA UTUKUFU KWA LIPI SASA? Unakumbuka habari ya Gidioni? Alidhani mpaka awe kwenye familia tajiri au awe mkubwa ndipo aweze kutumiwa na Mungu, kumbe Mungu alimridhia kwa hali yake ile ile kwa maana hata angekua vile alivyodhani ni bora, bila Mungu bado ingekua kazi bure. Kwani Goliati si alikua na vigezo vyote vya kibinadamu? Na Daudi si alikua hana vigezo vya kibinadamu? Lakini ni nini kilichotokea? UTUKUFU WA MUNGU SIKU ZOTE HUDHIHIRIKA KATIKA MAMBO MANYONGE NA MADHAIFU.

Maneno aliyoambiwa Gidioni, ndiyo Mungu anayosema nawe leo, kitabu cha WAAMUZI 6:14 Neno linasema

“BWANA, akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! si mimi ninayekutuma?”

MUNGU ni yule yule, hajabadilika. Anza kufanya hicho unachokihofia kwa uwezo wako huo huo, Mungu atajitwalia utukufu nawe utanyamaza kimya. (KUTOKA 14:14).

9. KUENDANA NA MABADILIKO.

Huwezi kuwa unataka mabadiliko lakini mambo yako na mienendo yako kiujumla ibaki vile vile. Kila hatua unayoipitia kuna mambo ambayo unahitaji, lakini pia kuna mambo ambayo ni adui wa maendeleo yako na kustawi kwako. Na si kwa habari ya mambo ya rohoni tu, hata mwilini pia. Kuna aina ya marafiki au watu ambao huwezi kuambatana nao. Yaweza kuwa si watu wabaya, lakini hawaendani na kile kitu ambacho Mungu ameweka ndani yako.

Na usilazimishe kuambatana na kila mtu, itakugharimu njiani. Pia Kuna tabia lazima uachane nazo, kuna aina ya mavazi ukilazimisha kuvaa yataua kile kilicho ndani na kuondoa utukufu wa Mungu. Usidhani mavazi hayazungumzi. Wewe kama ni askari vaa nguo zako za kiraia simama barabarani simamisha tu magari kiholela kama watu watasimama. Kila jambo ambalo unalifanya kwenye maisha yako ya kila siku hakikisha yanaendana na kile Mungu anataka ukifanye, au vile Mungu anataka uwe. Kama una maono ndani yako, kuna mambo lazima utaachana nayo upende usipende. Kwani MITHALI 29:18 inasemaje?

“Pasipo maono, watu huacha kujizuia, Bali ana heri mtu yule aishikae sheria.”

Je, wewe unajizuia na nini? Mambo ambayo unayafanya yanaendana na mabadiliko unayoyataka? Uwe tayari kujikana, uwe tayari kwa changamoto za kukufikisha viwango fulani bora zaidi ya hapo ulipo.






10. KUWA NA SHABAHA (TARGET).

Tatizo la watu wengi ni kupenda kufanya kila kitu au kubahatisha vitu. Lazima ujue Mungu hajakuumba kufanya kila kitu au kitu chochote, kuna eneo ambalo Mungu anategemea ulifanye kwa ukamilifu. Ni bora zaidi kumsihi Mungu akujulishe ni nini anataka ufanye, usipoteze muda kubahatisha mambo, wala usipoteze muda kufanya chochote au kila kitu.

Unajifunza nini kwa habari ya Dorkasi? Alielekeza nguvu zake na muda wake kwenye shabaha yake, soma (MATENDO 9:36-42) Alijua Mungu anataka afanye nini, na matokeo ya kile ambacho alikifanya kilionekana. Na njia mojawapo ya kujua unachokifanya ni sahihi kimetoka kwa Mungu au lah, ni yale matunda yanayopatikana. Usiwe mtu wa kuiga, usiwe mtu wa kulazimisha vitu kwakua fulani anafanya. Ipo neema, kibali na wepesi wa kufanya kile ambacho Mungu anataka ufanye. Na mambo hayo matatu ndiyo yanayotofautisha matokeo (matunda) kati ya mtu A na mtu B.

MUNGU AKUBARIKI SANA, NI OMBI LANGU KUPITIA SOMO HILI TULILOHITIMISHA, BWANA AFUNGUE MACHO YAKO UPATE KUJUA YAKUPASAYO KUTENDA.

Mwalimu Deborah E. Lema,

Mwalimu Deborah E. Lema (Mrs)
Delechancie@gmail.com
Facebook: Mwl Deborah Lema
S.L.P 179, Arusha
Piga +255-769-661628
Kujiunga na Group la Wanawake (KIZAZI CHA DORKASI),
ama Group la Wote (MPENYO WA ASUBUHI)
WhatsApp +255-657-578982

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni