Breaking

Jumanne, 2 Juni 2020

Somo : Nguvu Ya Neno La Mungu


Bwana Yesu asifiwe
Nakukaribisha tena siku ya leo ambapo tutajifunza Nguvu ya Neno la Mungu. Yohana 1:1-3 (Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.)



Maandiko yanaonyesha kuwa Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe na kupitia Neno la Mungu kila kitu kiliumbwa. Hata katika kuumbwa kwa ulimwengu ni Neno la Mungu ndilo lililotumika katika uumbaji Mwanzo 1:3 (Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.). Neno la Mungu lina uwezo wa kubadilisha maisha yako kwa kukutoa katika hali ya chini na kukuinua. Ili ufanikiwe katika maisha yako unatakiwa Neno la Mungu lijae kwa wingi ndani ya moyo wako. Hauwezi kufanikiwa katika maisha yako na hauwezi kushinda pasipo kutumia Neno la Mungu kwa kuwa Neno ni ushindi.Neno linaweza kufufua vitu vyote ambavyo vimekufa katika maisha yako.Ezekiel 37:5 (Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi) Mungu alisema na Ezekieli kuwa atoe unabii juu ya ile mifupa ili ipate kuishi,Ezekieli alifanya sawa na Neno la Mungu na hatimaye ile mifupa ikawa hai. Hakuna chochote kinachoshindikana mbele ya Neno la Mungu. Neno la Mungu lina uwezo wa kufanya lolote lile.

Ili ushinde katika changamoto yoyote unayopitia unatakiwa ujue Neno la Mungu linasemaje kuhusu hiyo hali unayoipitia,ukishajua hilo utaweza kumshinda shetani. Maisha yetu yote tangu mwanzo wetu hadi mwisho wetu yapo ndani ya Neno la Mungu kwa hiyo ili uishi katika mapenzi ya Mungu unatakiwa ujue Neno la Mungu.

Huwezi kumshinda shetani kama hakuna Neno la Mungu ndani yako.Shetani humshindi kwa nguvu zako, kwa Elimu uliyo nayo bali utamshinda shetani kwa Neno la Mungu. Mathayo 4:10-11( Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia). Bwana Yesu aliweza kumshinda shetani kwa Neno la Mungu pale alipojaribiwa.
Isaya 55:11 (ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.)Neno la Mungu huwa halirudi bure lazima litimie sawa na linavyosema.
Kwa hiyo kama Mungu amesema atakubariki ni lazima akubariki tu na hakuna cha kuzuia, kwa sababu Neno lake huwa halirudi bure.

Hakikisha Neno la Mungu linakaa kwa wingi ndani yako,pendelea kusoma Neno la Mungu kila siku na kulitafakari ili uweze kufanikiwa katika maisha yako na uweze kumshinda shetani. Asante sana na Mungu akubariki
                                       Contact: whatsapp +255756277095

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni