Breaking

Ijumaa, 28 Desemba 2018

Tambua Mambo 12 Yatakayokusaidia Katika Utumishi Wako Kwa Mungu


Bwana Yesu asifiwe,
Katika maombi yetu ya siku ya ijumaa, Mungu alituongoza kuombea utumishi wetu kwake. Wakati tunaomba, Mungu aliachilia vipengele vifuatavyo ambavyo vitatusaidia tuweze kusimama katika utumishi wetu.
Kitu cha muhimu kuliko vyote katika kumtumikia Mungu ni kutafuta kuyatenda mapenzi yake kama Bwana Yesu alivyofanya (Yohana 8:29). Kushindwa kuyatenda mapenzi ya Mungu katika utumishi kutafanya mtu asiingie katika ufalme wa mbinguni (Mathayo 7:21—23).

Pia ni muhimu sana kuelewa kwamba Mungu anapima utumishi wetu kwa “ubora” na siyo kwa “wingi.” (Mungu anaangalia “quality” na siyo “quantity.” Ulimwengu unaangalia “wingi” na siyo “ubora.”
Ulimwengu ukiona mtumishi anaweza kukusanya watu wengi, wanajua huyo ndiye ana “upako.” Yesu anasema njia pana ndiyo inayoenda upotevuni (Luka 13:24). Kumbuka kwamba injili ya kweli wakati wote inachoma na wengi hawataiendea (Yohana 6; Mathayo 10:34).
Mungu haangalii wingi wa watu ambao mtumishi anaweza kukusanya bali ni wangapi ambao wanafanywa kuwa wanafunzi wa Yesu. Maagizo ya Yesu ni kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake (Mathayo 28:18).
Hivyo kama uko kwenye utumishi wa aina yeyote, vipengele vifuatavyo vitakusaidia kusimama katika nafasi ambayo Mungu amekuweka ili umtumikie kwa uaminifu na kumzalia matunda. Yesu anachagua watumishi ili wamzalie matunda (Yohana 15:16).

1). USIIGE AU KUTAMANI UTUMISHI WA MWINGINE.
Hata siku moja usitamani upako wa mtumishi mwingine bali mtumikie Mungu kwa uaminifu mahali alipokuweka.
Kutamani utumishi au upako wa mtumishi mwingine kutakufanya utoke katika mpango wa Mungu na kutafuta kisichotokana na Mungu.
Unaweza kuona mtumishi anaonekana ana mafanikio kwa jinsi ya mwili lakini usielewe kinachoendelea katika ulimwengu wa roho. Bali endelea kumuomba Mungu akufunulie kile alichoweka ndani yako na mtumikie kwa hicho na utapata thawabu (Mathayo 10:42).

2). USIUPENDE ULIMWENGU.
Kuupenda ulimwengu kutakufanya uache kumtumikia Mungu. Paulo anaeleza jinsi Dema alivyomuacha kwa sababu aliupenda ulimwengu (2 Timotheo 4:10).
Pia mtu akiupenda ulimwengu hawezi kumpenda Mungu (1 Yohana 2:15). Kuupenda ulimwengu kunafanya mtu awe adui na Mungu (Yakobo 4:4). Kwa sababu hiyo, hawezi kumtumikia Mungu. Kuupenda ulimwengu ni pamoja na kupenda pesa (Mathayo 6:24).

3). FIMBO YA UTUMISHI.
Tafuta kujua maana ya fimbo ya Musa kugeuka nyoka mbele ya Farao na watumishi wake. Fimbo ya Musa ilikuwa inawakilisha utumishi wa Mungu ndio maana Biblia inasema ilikuwa “fimbo ya Mungu” (Kutoka 4:20).
Pia tunaona jinsi fimbo ya Haruni ilivyochipua kuwakilisha utumishi ambao Mungu amempa (Hesabu 17:8). Ila tafuta kujua kitendo cha fimbo ya Musa kugeuka nyoka kwani kuna siri kubwa sana hapa juu ya utumishi.

4). MUSA KUMUINUA NYOKA JANGWANI.
Neno linasema, “Musa akafanya nyoka wa shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi” (Hesabu 21:9).
Tafakari hayo maandiko juu ya utumishi wa Musa. Katika utumishi wa Bwana Yesu, neno linasema, “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa” (Yohana 3:13—14).
Tafakari hayo maandiko ili Mungu akufunulie jinsi Bwana Yesu atavyokwenda kuinuliwa kupitia utumishi wako na jinsi ambavyo Mungu ataokoa watu kupitia utumishi wako kama alivyofanya kwa Musa.

5). AHADI YA KRISTO KWA WATUMISHI WAKE.
“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataita yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:18—20).
Endelea kumtumikia Kristo katika uaminifu naye hatakuacha (Yohana 14:18).

6). DHIKI INAKUJA.
Mungu ataacha tupitie dhiki na mateso lakini atatusaidia kuyashinda yote kwa ajili ya utukufu wake. Mathayo 10:17—31; Matendo 20:22—23; Wafilipi 4:12—13.
7). USITAFUTE KUWA MAARUFU.
Usitumie utumishi kutafuta kujulikana au kupata umaarufu bali tumia utumishi wako kumuinua Kristo. Hivyo usinene yaliyo yako, bali yaliyo ya Kristo (Yohana 7:18).

8). USITAFUTE KUKUBALIKA KWA WANADAMU.
Usitafute utukufu wowote kwa wanadamu. Mtu yeyote ambaye anatafuta kukubalika kwa wanadamu, hawezi kumpendeza Mungu.
[Yesu] “Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaoidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele ya Mungu” (Luka 16:15).

9). HUBIRI/FUNDISHA KILE AMBACHO MUNGU AMEKUAMBIA.
Katika mazingira yoyote, usihubiri kitu ilimradi uhubiri. Bali wakati wote nenda mbele za Mungu ili kupata maelekezo. Watoto wa Mungu wakati wote wanaongozwa na Roho Mtakatifu (Warumi 8:14).
 Kuna watumishi ambao wanaangalia mahitaji ya watu halafu wanawaletea maneno/masomo kutokana na kile wanachotaka kukisikia na hivyo kuwadanganya (Yeremia 28:1—17; Yeremia 29:24—32).
 
10). USIBADILISHE INJILI.
Haijalishi mazingira uliyonayo, hata siku moja usilitengue neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo ya wanadamu kama walivyofanya mafarisayo (Mathayo 15:3).
Usipunguze/kuongeza neno kwa ajili ya watu. “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndugu, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu akayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 19).

11). JITENGE NA MADHABAHU ZA UONGO.
Usijiunganishe na madhabahu au mtumishi yeyote pasipo kuongozwa na Mungu. Hii imeuwa utumishi wa watu wengi.
Kwa mfano, kuna watu ambao Mungu aliweka huduma ya unabii ndani yao na wakajiunganisha na manabii wakubwa wa uongo pasipo kujua na hivyo utumishi wao kufa.
Kilichoua utumishi wa Balaam ni kujiunganisha na Balaki (Hesabu 22—24). Hiki ni kipengele muhimu sana kwa ujumla kwani siyo kila madhabahu inayomtaja Yesu ni Mungu wa kweli.
Kuna utapeli mwingi sana ambao unaendelea na watu wengi wamevaa mavazi ya utumishi lakini kumbe ni mbwa mwitu wakali, wezi, wanyang’anyi (Mathayo 7:15; Yohana 10:10).
Biblia imeonya juu ya wale ambao wanatumia utumishi kwa ajili ya faida yao na tumbo ndio mungu wao (Wafilipi 3:19; 1 Timotheo 6:3—5).
Pia kuna watumishi ambao wanatumia nguvu za giza. Sasa fikiria kitu gani kitatokea kama ukiwekewa mikono na mtumishi wa aina hii au ukijiunganisha na madhabahu hiyo.
Hivyo ingia kwenye maombi na muombe Mungu akuonyeshe kinachoendelea katika madhabahu yoyote ile ambayo kwa namna moja au nyingine unajihusisha nayo. (ikiwa ni pamoja na hii).
Kuna madhabahu zimeua utumishi wa watu pasipo wao kujua. Na kuna zingine zimesaidia watu watambue utumishi wao.

12). NGUZO 12 ZA UTUMISHI.
Tafuta kujua uhusiano uliopo kati ya Ufalme wa Mungu na namba 12. “… Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa” (Ufunuo 12:2)
Hapa ndipo utajua kwanini Yesu alichagua mitume 12. Pia tafuta vitu 12 tofauti vya kiutumishi vilivyopo kwa wale watoto 12 wa Yakobo. Tafuta kujua sifa za Yusufu, Rubeni, Gadi, Asheri, na wengine wote.
Kila mmoja ana kitu cha tofauti cha kiutumishi ambacho Mungu anataka tukifahamu (pamoja na kwamba siyo wote waliotembea katika mapenzi ya Mungu).
Ubarikiwe,
Jacob & Devota Makaya
Kingdom of Heaven Ministry

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni