Mpendwa katika Bwana ni ombi langu kwa Mungu akubariki unaposoma somo hili ili uweze kufahamu mambo ambayo ulikuwa huyajui au kukumbuka yale ambayo unayajua lakini ulikuwa umeyasahau.
Kipengele hiki kidogo cha somo hili nimekitoa katika makala niliyoiandaa na hivyo, ni tamanio la moyo wangu kuwa litaeleweka vizuri kama somo lililokamilika kwa lengo hili na kwa wakati huu. Kama wewe ni mwanamuziki, mwimbaji au mdau wa muziki, basi naamini utapata jambo la kujifunza kwa kipindi hiki unaposoma.
Muziki, pasipo kujali unatumikaje, kitaaluma huwa uko katika eneo la Sanaa. Vitu vyote vyema vinatoka kwa Mungu (Yakobo1:17). Tunafahamu kuwa vitu vyote tulivyonavyo chanzo chake ni Mungu mwenyewe na vikitumika vyema, huonyesha sura fulani ya Mungu wetu. Hivyo mwana sayansi mkuu ni Mungu na mwana sanaa mkuu pia ni Mungu mwenyewe.
Mungu kama mwana sanaa alipanga vitu vyote katika picha na kama mwana sayansi akatumia sayansi na sanaa kuviumba na kuviweka viwepo hata leo. Naamini kupitia sanaa ya Mungu, ndipo usemi maarufu wa Biblia, “Mungu akaona yakuwa ni vyema” ulirudiwa mara kwa mara katika kitabu cha Mwanzo.
Saana ina uwezo mkubwa sana kuunganisha vyema vitu visivyoonekana wala kusikika na kuvileta katika ulimwengu unaoonekana na kusikika. Mchoraji anaweza kuunganisha mistari na kuonyesha picha ya kitu fulani. Hivyo hivyo, mwana muziki au mwimbaji anaweza kuweka nota na milio tafauti tofauti na kutengeneza wimbo au muziki unaosikika vizuri.
Ni jambo la ajabu sana kuwa neno ‘Msanii’ limetumika vibaya sana katika sehemu hii ya dunia tunayoishi kufikia wasanii kuanza kuchukia kuitwa/kutambulishwa hivyo. Hata hivyo, ingekuwa ajabu pia kwa Ndovu kukataa kuitwa Ndovu kwa kukuta Fisi akiitwa Ndovu. Daktari hawezi kukataa kutambulishwa kama Daktari kama jina Daktari litatumika vibaya. Kwa nini Msanii akatae kuitwa hivyo kwa sababu jina hilo limetumika vibaya?
Kwa hivyo, Msanii katika Kanisa lazima ajivunie kuwa Mungu amempa huduma ya kutumia Sanaa hiyo kumtumikia kama vile Injinia anavyoweza kujivunia kutumia taaluma yake ya ujenzi kwa ajili ya kujenga nyumba ya kuabudia Mungu. Mungu ameweka Sanaa ya Muziki ili utaalamu huo utumike kuleta sifa nyumbani mwake. Kwa maana hiyo, ni vyema wana muziki wakajitahidi kukuza taaluma hiyo kwa elimu ya kiroho na ya asili pia inayohusu muziki.
Ki ujumla, sanaa hutumia uwezo wa kuwaza, kufikiria na kutumia (imagination)
kwa upana sana, ambako huleta picha hiyo kuonekana au kusikika. Tofauti na taaluma nyingine, sanaa hutumia ubunifu(creativity) mwingi kwa sababu sheria na kanuni zake hazijabana sana tofauti na sayansi ambayo kanuni zake na mahesabu yake yako ya ki-vipimo zaidi. Hivyo, sanaa ina uwezo wa kubuni mambo mapya sana. Kwa mfano, muziki wa Jazz ulipobuniwa na watu weusi huko Marekani, watu walipinga uhalali wake huku wakisema kuwa kanuni za ki-muziki zimevunjwa. Lakini baada ya muda, muziki wa Jazz uliongezeka umaarufu wake na baadae ukakubalika kuwa muziki halali.
Muziki kama sanaa nyingine hutumia hisia nyingi ili kufikia walengwa. Kwenye taasisi tatu za mtu, yaani roho, nafsi na mwili ambazo humfanya mwanadamu kuwa mwanadamu, nafsi hutumika kwa asilimia kubwa sana kufanya kazi ili kutengeneza na kuhudumu katika sanaa. Katika nafsi, kitengo cha hisia ndicho kinachofanya kazi kubwa ya ziada kufanya sanaa,(sisi hapa tukihusika na muziki.) Kwa hivyo tunapoenda kuongea muziki moja kwa moja, tunafahamu kuwa mambo mengi yanayowaathiri wana muziki na waimbaji, basi yanaathiri wana sanaa kwa ujumla wake.
Naamini kuwa wote tunakubaliana kuwa wanamuziki na waimbaji ni watu wa hisia nyingi. Ndivyo Mungu alivyowaweka duniani ili watumike kufariji, kufurahisha na kuonyesha huzuni ili kuhudumia jamii. Kwa sababu ya hisia nyingi zinazotumika katika muziki, wakati mwingine, ni rahisi kwa wanamuziki na waimbaji hawa kukosa mwelekeo, mizani na vipimo(balance), wingi au upungufu wa hisia unapotokea. Jinsi ya kujitunza ki-hisia huwa ni jambo la muhimu sana, jambo ambalo wengi wao hawajui, ili wasije wakafanyika kituko badala ya suluhisho katika jamii.
Kupitia hisia na sehemu kubwa ya mchango katika maisha ya mwanamuziki na mwimbaji, itaonekana jinsi ya kuvaa na staili zake za maisha kwa ujumla zilivyo tofauti sana na za watu wengine katika jamii. Hapa, hatuwezi kuwaambia wabadilike wasiwe hivyo, maana mara nyingi hicho huwa ni kitambulisho cha taaluma yao, ila wanahitaji tu kudumisha kiasi tu, ili wasipitilize, na pia wasifanye kwa kuiga.
Sasa, mtu yeyote anayetoa huduma katika jamii, lazima ajifundishe kurudisha katika maisha yake kile kinachotoka anapohudumia jamii ile. Kwa mfano, mwana riadha anahitaji ale chakula kizuri, apumzike, ajiweke vizuri kisaikolojia ili asihudumie jamii na baadae maisha yake yakaharibika. Anapofanya mazoezi na hatimae kushindana, anahitaji ajue ni chakula gani cha kutumia ili arudishe nguvu na kadhalika. Mtumishi wa kiroho, kama mchungaji anahitaji aombe na kuabudu Mungu, asome neno na kuwa na ushirika mzuri na pia kupumzika ili arudishe nguvu anazotumia katika huduma yake. Vile vile, mwanamuziki na mwimbaji wa nyimbo za injili lazima ajue jinsi ya kurudisha nguvu anayotumia ikiwemo ya kihisia ili aweze kuhudumu bila maisha yake mwenyewe kuharibika.
Huduma ya muziki na uimbaji ina shamrashamra nyingi, makelele mengi na kuhudumia mbele ya umati au watu wengi. Ni rahisi jambo hili likaingia vibaya katika akili ya mwimbaji au mwanamuziki huyo na kuanza kuishi katika ‘ulimwengu’ usiyo halisi.
Ile kushangiliwa na muonekano wa kugusa umati au watu wengi unaweza ukaweka picha isio ya halisi katika maisha ya mtu huyo na akaanza kuishi maisha tu ya juu juu. Ikumbukwe kuwa mwanamuziki na mwimbaji wa nyimbo za Injili ni mwanadamu na hivyo ana mapito yake katika maisha. Tafakari sasa kuwa amekuwa na wakati mbaya katika maisha yake na sasa ana huzuni lakini hapo hapo anatakiwa kusimama mbele za watu na kuwafurahisha au kuwatia moyo.
Anatakiwa hapo hapo atumie hisia yake kuwafurahisha watu wakati yeye mwenyewe ki-hisia yuko chini. Pasipo Mungu kuwa naye na kumsaidia katika huduma yake, hali hii inapotokea mara kwa mara, inaweza ikamchanganya ki-hisia. Kwa sababu ya umuhimu wa hisia katika maisha ya mwanadamu yeyote, hisia zinapochanganyikiwa, mwanadamu hujikuta katika ulimwengu usiyo halisi na kuwa kituko katika jamii, huku yeye akiona kuwa yuko sawa.
Kwa nini Neno ‘Msanii’ limetumika vibaya?
Kwa nini neno Msanii limetumika kuonyesha utovu wa maadili? Ningependa (nikiwa na uchungu mwingi moyoni) kuangalia sababu ya jina Msanii kutumika kuonyesha sifa mbaya katika jamii. Hili linaniumiza kwa sababu na mimi nina taaluma ya sanaa. Imekuwa tabia ya watu wengi katika sehemu hii ya ulimwengu tunayoishi kutumia neno hili kuonyesha mtu tapeli, muongo asiyeeleweka na kadhalika.
Sifa ya sanaa ni kuonyesha picha ya kitu kilichopo au ambayo msanii anataka kuitengeneza ili ionekana kama wazo katika jamii. Kwa mfano, msanii mwimbaji anaweza kutumia sanaa kukuonyesha mambo yaliyopo katika jamii. Anaweza kuimba wimbo wenye hadithi ya fulani hata kama sio picha halisi ya maisha yake. Anaweza kuimba wimbo kuwa anataka kuolewa na kupata watoto wengi hata kama kihalisi hataki hata mtoto mmoja.
Mwimbaji anaweza kukupa picha ya maisha ukafikiri kuwa ndivyo alivyo, kumbe sivyo hivyo. Kupitia hili, Msanii ameonekana kama kuwa mwongo fulani hivi. Ameonekana kama mtu anayeweza kuichora picha yoyote na kujionyesha mtu ambaye siye katika jamii.
Muziki umetumika kujibizana na hata kugombana na kutukanana, mwimbaji mmoja na mwingine. Mambo ambayo yameleta picha ya sanaa kutumika kuwa chombo cha (kumfagilia) kumsafishia jina msanii husika. Kwa sababu ya nguvu ya sanaa, wasanii wengi wameitumia kwa faida binafsi kujitengenezea nafasi katika jamii, badala ya kuihudumia jamii ile.
Kwa sababu hapa tunaangalia sanaa ya muziki katika nyumba ya Mungu, ni vyema tutoe tahadhari kuwa Muziki wa Mungu unatakiwa kumtukuza Yeye, kuhudumia kundi lake na kusaidia kuleta wengi katika kundi hilo.
Muziki na vipawa vyote katika nyumba ya Mungu vinatakiwa kutumika kwa utukufu wa Mungu na hivyo sio kwa ubinafsi. Kwa sababu hiyo wanamuziki katika nyumba ya Mungu wasiwe kama wa dunia ambao wanaimba nyimbo kuhamasisha jamii kuhusu jambo moja huku wao wakifanya kinyume.
Mwanamuziki au muimbaji wa Mungu asiimbe kuwa yeye anapenda kuomba wakati sio kweli maana hapo ndipo atakapoonekana na watu kuwa ‘Msanii’ kwa kinyume cha matumizi ya jina hilo. Hili limeonekana kwa watu wengi wanaoimba nyimbo za injili na za kusifu na kuabudu kuwa wanachoimba na wanachofanya ni vitu viwili tofauti.
Mungu asaidie ili neno hili linapotumika kinyume duniani, katika nyumba ya Mungu Msanii awe ni chombo cha heshima cha kumtukuza Mungu na si vinginevyo.
Jambo lingine ambalo hufanya neno ‘Msanii’ kutumika vibaya ni kwa sababu ya kitu ambacho nimegusia awali kuwa, wengi wao huchanganyikiwa kwa kuzidiwa namsongamano wa hisia katika maisha yao na hivyo kuonekana kuishi maisha yasio halisi, na hivyo mtu yeyote anayeonekana kudhihirisha aina hii ya maisha hufananishwa na wasanii waliofanyika hivyo. Hivyo huonekana kama vile ndio maisha ya wasanii kuishi katika maisha ambayo sio ya kawaida na watu wengine, kwa kuvaa kwao labda na hali zingine ambazo huonekana maishani mwao.
Wanamuziki na waimbaji wanaohudumu katika nyumba ya Mungu wanatakiwa kuonyesha mfano katika maisha yao ili waonekane kuwa ni wahudumu zaidi kuliko tu kuonekana kuwa ni waimbaji, kwani vipawa vyao vinatakiwa kudhihirisha tabia fulani ya Mungu. Njia ya kufuta dhana hii katika waimbaji na wanamuziki walio katika nyumba ya Mungu ni kushinda majaribu ambayo huwalenga na kuishi kwa Imani zaidi kuliko kihisia, kwani, Biblia inasema tunaishi kwa Imani na sio kwa yale tunayoyaona na kuyahisi. Kwa hivyo wajenge nguvu ya kiroho katika maisha yao na waongozwe na Roho Mtakatifu.
Jambo jingine ni kuomba uongozi wa Mungu kwa Roho Mtakatifu ili nyimbo zao ziwe zinatokana na njaa na kiu ya Mungu na haki yake katika maisha yao, ili wasije wakaimba nyimbo ambazo wanawaelekeza watu wafanye yale ambayo wenyewe hawayafuati.
La mwisho, katika somo hili, ni kuomba kipawa chao kiambatane na neema iliyo juu ya maisha yao ili kipawa kisiwapeleke juu zaidi kuliko neema inayoweza kuwalinda katika kiwango hicho. Pia waweze kuwa na afahamu wa kujua milango inayofunguka kwao, kama ni Mungu aliyefungua au ni wanadamu maana mara nyingi hapo ndipo watu hupandishwa na kujikuta mahali ambapo hakuna neema ya kumlinda mtu katika kiwango alichopandishwa. Hivyo wawe pia na ujasiri wa kufuata tu njia ambayo Mungu anatengeneza.
Muziki una nguvu yake wenyewe, Ni jambo la muhimu kujua kuwa Muziki kama Muziki una nguvu ya ajabu sana, ukiachilia mbali kuwa unaweza kuubeba upako. Kwa maana nyingine, muziki una uwezo ndani yake wa kujitegemea bila kujali ni nani anayeutumia. Muziki una nguvu kwa sababu ya asili ya ulivyoumbwa. Kama chombo cha mawasiliano, kuna uwezo ndani ya muziki ambao husaidia kuleta ujumbe katika jamii lengwa. Labda kwa sababu hii, ndio maana huduma ya muziki na uimbaji imebeba umuhimu mkubwa sana nyumbani mwa Mungu. Inawezekana umuhimu mkubwa ni ukubwa wa muziki wenyewe na sio tu kutokana na wana muziki na waimbaji wenyewe. Kwa sababu hii, watu walio katika huduma hii wanaweza kujibebea heshima kubwa bila kujua kuwa chombo chenyewe ndicho muhimu kuliko wenyewe.
Muziki ni chombo cha muhimu sana katika uumbaji wa Mungu kwa hiyo kinabeba nguvu nyingi sana na hivyo kinatumika kwa ajili ya kuleta mabadiliko makubwa sana katika uumbaji mwingine wa Mungu. Kipawa cha muziki, kina uwezo wa kumuonyesha mwanamuziki na muimbaji katika hali fulani ambayo asipojiangalia, anaweza akajitafsiri katika hali ambayo sio halisi katika maisha yake. Anaweza kujisifu na kujiona yuko katika kiwango fulani cha ki-maisha ambacho sio halisi katika maisha yake, kumbe tu ni kwa sababu ya nguvu iliyo katika muziki wenyewe.
Hata hivyo, nguvu ya muziki iko sana katika kugusa hisia za nafsi, na hivyo kutegemea nguvu ya kiroho kuleta mguso katika maisha ya kiroho. Katika muziki, maisha ya watu wanaohudumiwa, wanaweza kuguswa katika kiwango cha ki-hisia tu au, wakaguswa katika kiwango kingine, wakafikiwa katika maisha ya kiroho.
Sasa hapa ndipo tunapogundua umuhimu wa kipawa au talanta ya muziki kushukiwana kipawa au karama ya kiroho. Wako wanamuziki wengi wa duniani kwa kujua hili wanatafuta nguvu za giza kwa kwenda kwa waganga/wachawi au hata kutafuta kuabudu mashetani ili wawe na mguso wa kiroho. Sisi tulio katika nyumba ya Mungu tunatafuta kwa Mungu uwezo na vipawa vya kiroho ili karama ishuke juu ya talanta na hivyo kugusa, sio tu nafsi na hisia zake bali roho ya mtu au maisha yake ya kiroho. Kipawa cha kimwili(talanta/kipaji) hakiwezi kugusa rohoni. Kipawa cha kiroho(karama) hugusa rohoni. Kwa hivyo vyote ni muhimu, ila tunajua kuwa vitu vya kimwili ni vya muda na vya kiroho ni vya kudumu.
Kuna mifano mingi katika Biblia ambayo inaonyesha talanta za ki-muziki ambazo zilishukiwa na karama za rohoni. Tunafahamu hadithi ya Daudi katika 1Samueli 16:23“Ikawa ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa na, na ile roho mbaya ikamwacha.” Hapa kuna ufunuo mwingi sana. Kwanza, muziki ulimburudisha Sauli, kama vile tulivyoona hapo juu kuwa muziki una nguvu wenyewe na la pili, Sauli aliondokewa na roho mbaya, ambayo ni kipawa au karama ya kiroho ambayo ilifanya kazi hiyo.
Pia kuna wazo hilo la ‘roho mbaya kutoka kwa Mungu’ ambapo watumishi wengi hutafsiri kuwa ni roho iliyoruhusiwa na sio kuwa ilitoka kwa Mungu wakisema kuwa Mungu hana roho mbaya. Wengine pia husema ni aina ya roho ya ghadhabu ambayo inatafsirika kuwa ni mbaya. Hata hivyo la muhimu kujua hapa ni kwamba ukombozi ulitokea kwa Sauli wakati Daudi alipopiga muziki.
Andiko jingine ni pale Nabii Elisha alipohitaji mwanamuziki katika 1Wafalme 3:14-15. “Elisha akasema, Kama Bwana wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe. Ila, sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga mkono wa Bwana ukamjia juu yake. Akasema, Bwana asema hivi……..” Hapa, kuna hadithi ya nabii ambaye amekwazika kumuona adui ambaye alikuwa mfalme muovu. Lakini kwa ajili ya Yehoshefati, Elisha akaheshimu uwepo wake na akaomba mwanamuziki ambaye alipopiga muziki ule, upako ukaja juu ya Elisha na akatabiri. Hapa tunaona talanta/kipaji ya muziki ikishukiwa na karama ya unabii ambayo ilifanya kazi juu ya nabii Elisha. Kwanza nguvu ya muziki ilimuondolea Elisha kukwazika kwa kumfurahisha na pili, karama ya unabii ilichochewa na karama iliyokuwa juu ya mwanamuziki yule.
Na mwisho, kwa sasa katika mifano, tunaona katika 1Mambo ya Nyakati 25, mara kwa mara ikisemekana kuwa wana muziki waliochaguliwa na mfalme Daudi na viongozi wa kiserikali walipewa kazi ya kutabiri kupitia muziki, katika mstari wa 2, “…..walioamriwa na Asafu aliyetabiri kwa amri ya mfalme” na mstari wa 3, “…..watu sita; walioamriwa na baba yao Yeduthuni mwenye kinubi, aliyetabiri katika kumshukuru na kumsifu Bwana.” Wana muziki na waimbaji wanatakiwa kuheshimu kuwa Mungu amewapa talanta za kumtumikia Yeye, lakini pia watafute karama za Roho Mtakatifu ili wanapogusa watu wa Mungu, basi iwe katika maisha yao yote kwa ujumla.
Ninaamini kuwa Mungu amekupa kitu chema cha kukusaidia ili uweze kutoa mchango wako katika huduma hii kwa ajili ya kuiboresha.
Hadi wakati mwingine tutakapowasiliana tena, Ni mimi wako katika shamba la Mungu.
Pastor Willy Mshila.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni